Thursday, January 2, 2014

Wawili wadaiwa kutelekeza begi la pembe za Tembo



Na Mussa Mwangoka, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Januari2  2014  saa 10:37 AM
Kwa ufupi
  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea Desemba 24, mwaka jana  saa 2:30 usiku Kijiji cha Kabungu, barabara  inayotoka Mpanda kuelekea mkoani Kigoma.
Sumbawanga. Watu wawili wanaosadikiwa ni majangili wametelekeza  begi  moja likiwa na vipande saba vya pembe za Tembo,  vyenye uzito wa kilo 19 vikiwa na  thamani ya zaidi ya Sh45 milioni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea Desemba 24, mwaka jana  saa 2:30 usiku Kijiji cha Kabungu, barabara  inayotoka Mpanda kuelekea mkoani Kigoma.
Kidavashari alisema siku  ya tukio polisi waliokuwa  doria waliwaona watu hao wakiwa wamepakia beji kubwa jeusi  kwenye pikipiki aina ya SanLg, waliwatilia mashaka watu hao na kuanza kufuatilia nyendo zao.
Alisema wakati wakifuatilia  walipata taarifa za raia wema kwamba, watu hao walikuwa na nyara za Serikali kinyume cha sheria hivyo jitihada za kuwanasa zilianza kwa kuandaa mtego.
Kidavashari alisema polisi waliokuwa wameandaa mtego wa kuwakamata, watuhumiwa waliposimamishwa waligoma.
Alisema hali iliyolazimu polisi kuanza kuwafukuza, walipogundua wanafuatwa na askari waliacha  njia na kuingia kwenye kichaka na kutoweka huku wakitelekeza  begi jeusi ambalo lilikuwa na vipande hivyo vya pembe za Tembo na  pikipiki waliyokuwa wakitumia.
Kamanda Kidavashari alisema  baada ya polisi kufanya upekuzi  kwenye beji hilo, walikuta vipande saba vya pembe za Tembo vyenye uzito wa kilo 19 vya thamani hiyo ya fedha.

No comments:

Post a Comment