JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAARIFA
KWA UMMA
Itakumbukwa kuwa Serikali iliamua kuanzisha “Operesheni
Tokomeza Ujangili” kufuatia kukithiri kwa vitendo vya ujangili katika maeneo
yote yaliyotengwa kisheria kama Mapori ya Akiba; Hifadhi za Taifa na Hifadhi za
Misitu katika miaka ya karibuni. Hata hivyo, Serikali iliamua kusitisha
operesheni hiyo kwa muda.
Kufuatia kusitishwa kwa Operesheni Tokomeza, matukio
ya uvunjaji wa sheria za hifadhi kama vile uingizaji holela wa mifugo katika
maeneo ya hifadhi; ujangili wa tembo pamoja na uvunaji wa miti katika hifadhi
za misitu yanaonekana kushamiri. Aidha, kumekuwa na
ongezeko la kuvamiwa watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na hata
kuwasababisha madhara yakiwemo vifo na majeraha. Baadhi ya matukio hayo ni
pamoja na:
·
Majangili kuua takriban tembo 60 katika
Hifadhi/Mapori ya Selous, Rungwa, Burigi na Katavi na Ngorongoro. Hawa ni
takriban tembo wawili kwa siku. Ikumbukwe kuwa wakati wa kipindi chote cha
operesheni kilichodumu kwa mwezi mmoja ni tembo wawili tu waliokuwa wameuawa.
·
Watumishi wa Pori la Akiba Mkungunero (Kondoa) waliokuwa
doria kuvamiwa na kundi la watu wapatao 80 waliokuwa na mikuki na silaha
nyingine za jadi tarehe 24 Desemba, 2013.
·
Kuuawa kwa Askari mmoja wa wanyamapori
aliyejulikana kwa jina la Ramadhani Magengere (40) na mwingine, Bwana Yahaya
Ramadhani (34), kujeruhiwa vibaya na Wafugaji walioingiza mifugo ndani ya
Hifadhi ya Wanyamapori ya Jumuiya (WMA) Ukutu (au JUKUMU) iliyoko Morogoro
vijijini tarehe 6 Decemba, 2013.
·
Mtumishi mmoja wa wanyamapori, Sajidi Majidi,
kujeruhiwa kwa kuchomwa mkuki kichwani na kuvunjwa mkono na wafugaji walioingiza
ng’ombe katika Eneo la Ramsar la Kilombero tarehe 14 Novemba, 2013.
·
Kukamatwa kwa gari lililokuwa na mizoga 20 ya
swala wilayani Simanjiro siku za karibuni
·
Kuanzishwa kwa kambi ya majangili katika Pori la
Akiba Burigi ambapo vitendo vya ujangili vinaendeshwa. Majangili waliokuwa na
silaha za moto walikimbia na kuacha nyuma nyani 30 waliokuwa wamewaua baada ya
kukurupushwa na askari wa wanyamapori.
·
Kuongezeka wimbi la uvamizi na ufugaji wa mifugo
ndani ya mapori ya akiba na hifadhi za misitu iliyopo magharibi mwa nchi yetu,
hasa Burigi-Biharamulo-Kimisi, malagarasi-Moyowosi, Rukwa Lukwati, Luwanda,
Ugalla, Ibanda-Rumanyika, Minziro na Katavi.
Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda
kuwakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka
2009 pamoja na Sheria zinazosimamia maeneo ya Hifadhi za Taifa na Misitu kuwa
hairuhusiwi wananchi kuingia katika maeneo haya bila kibali ikiwa ni pamoja na
uingizaji wa mifugo kwa ajili malisho. Aidha, bado vitendo vya ujangili
haviruhusiwi chini ya sheria hizi. Kifungu cha 15 ni marufuku mtu yeyote
kuingia kwenye pori la akiba bila kibali.
Aidha, Sheria hiyo inakataza kuwa na silaha yoyote ndani ya Pori la
Akiba bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori [kifungu cha 17]; kuwinda,
kuua, kukamata au kujeruhi mnyama [Kifungu cha 19] na kuchunga ng’ombe ndani ya
Pori la Akiba [Kifungu cha 21].
Ikumbukwe kuwa matukio yaliyotokea bungeni
Dodoma, hayajatengua Sheria yoyote ya Wanyamapori au Misitu. Hamna maamuzi yoyote ya Bunge yaliyohalalisha
ukiukwaji wa Sheria za Uhifadhi. Hivyo, wananchi wanatakiwa kutii na kufuata
Sheria hizo kama zilivyo. Tahadhari inatolewa kuwa Serikali haitasita
kumchukulia hatua kali yeyote atakayekiuka Sheria ya Wanyamapori kwa makusudi.
Tunawaomba wananchi wasikubali kudanganywa na mtu yeyote yule kuvunja Sheria za
nchi.
Aidha, nachukua nafasi hii kuwaagiza watumishi
wote wa Wizara ya Maliasili na Utalii wahakikishe kuwa wanaendelea kutekeleza
majukumu yao ya ulinzi wa maeneo ya Hifadhi za Taifa, Mapori ya Akiba na Misitu
ya Hifadhi bila kutetereka. Sanjari na hilo wasisite kuchukua hatua stahiki
dhidi ya mhalifu yeyote mradi tu wanazingatia Sheria, Kanuni na taratibu. Utekelezaji huu wa sheria ufanyike bila
kuathiri haki za msingi za binadamu.
Serikali ina maadili na miiko inayotawala
utendaji kazi wa watumishi wake wote wakiwemo wale wa maliasili. Wizara ya
Maliasili itaendelea kuwakumbusha watumishi wake juu ya maadili na miiko hii
kupitia mafunzo ya mara kwa mara na mbinu nyingine. Aidha, Wizara itaendelea
kuboresha miongozo inayohusu maadili na miiko hii ili iweze kuendana na wakati.
Mwisho, Serikali inasisitiza kuwa, kwa kutumia
vyombo vyake, itaendelea kutekeleza majukumu yake na kusimamia ipasavyo Sheria
ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayeshiriki moja kwa
moja au kusaidia vitendo vya ujangili ili kunusuru rasilimali za Taifa. Jukumu
la uhifadhi wa maliasili zetu liko pale pale, ni letu na lazima litekelezwe kwa
manufaa ya kizazi hiki na vizazi vijavyo.
Imetolewa na:
Mh. Lazaro Nyalandu, MB.
NAIBU
WAZIRI, MALIASILI NA UTALII
Desemba
29, 2013.
No comments:
Post a Comment