Kwa ufupi
Uamuzi huo ulitangazwa jana na naibu waziri katika wizara hiyo,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii, imewasimamisha kazi watumishi wake 21
kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia ujangili wa nyara za
Serikali.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Polisi mkoani Singida, kumkamata
ofisa wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, kwa tuhuma za
kupatikana na silaha mbili na nyara za Serikali, kinyume cha sheria.
Akitangaza hatua hiyo jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema Serikali inasikitishwa na vitendo
viovu vinavyofanywa na watumishi wake na haitavivumilia. “Tumesikitishwa na
kitendo cha ofisa wanyamapori wilayani Singida kukamatwa na bunduki mbili na
ndege aina ya Heroe 12 nyumbani kwake, hatua tuliyochukua ni kumsimamisha kazi
na kufikishwa mahakamani,” alisema na kuongeza:
“Wizara baada ya kufanya uchunguzi, imegundua kuwa kuna watumishi
wanaoshirikiana na mtandao wa ujangili, hivyo imewasimamisha kazi watumishi 21
wa Idara ya Wanyamapori na tutachukua hatua zaidi.”
Alisema kati ya watumishi hao, 11 wanatoka katika Kikosi cha Kuzuia
Ujangili mkoani Arusha, wanne wanatoka Mkoa wa Rukwa katika Pori la Akiba la
Lwafu, mmoja Kikosi cha Bunda, watatu Pori la Akiba la Maswa, mmoja Selous, na
mwingine mapori ya Lupika, Lumesule na Lusangu.
Akifafanua kuhusu uhaba wa watumishi katika Idara ya Wanyamapori,
Nyalandu alisema kwa zaidi ya miaka 10 wizara hiyo haikuwa ikiajiri watumishi
hali inayosababisha kukosa watumishi wenye ujuzi.
“Tunajipanga kuajiri watumishi wengine wenye ujuzi na kuangalia
maendeleo ya teknolojia hasa kwa kujifunza kwa wenzetu Afrika Kusini,” alisema.
Kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, alisema Serikali imeunda tume ya
kimahakama itakayowahoji askari waliohusika na kurudisha taarifa. Hata hivyo
alisema wako mbioni kuendelea nayo.
“Rais Jakaya Kikwete ameunda tume ya kimahakama na itatoa taarifa, ila
sisi hatutalala, tutahakikisha kuwa tunapambana na ujangili ili kulinda nyara
za Taifa,” alisema Nyalandu.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wizara yake kwa kutoa taarifa
zitakazowezesha kuwakamata wahalifu.
“Jitihada hizi siyo zetu wenyewe, tunashirikiana na vyombo vya ulinzi na
usalama. Tunawaomba wananchi washirikiane kulinda na kutoa taariza
zitakazowezesha kukamatwa kwa wahalifu. Tunawaomba watumishi wetu wafanye kazi
kwa moyo na uaminifu,” alisema Nyalandu.
Mamlaka ya wanyamapori
Akiwa katika pori la akiba la Selous hivi
karibuni, Nyalandu alieleza mkakati wa Serikali wa kuanzisha mamlaka ya
wanyamapori ili kuwapa mamlaka watendaji wa sekta hiyo katika kutunza
maliasili.
No comments:
Post a Comment