Saturday, January 4, 2014

Mwaka 2013; uliacha ‘vilio’ kwa tembo


Baadhi ya matukio yaliyowahi kuripotiwa ni pamoja na baadhi ya watumiaji silaha katika sekta ya ulinzi na usalama nchini wakiwamo askari huzikodisha silaha zao kwa ajili ya kutumika katika matukio ya uhalifu.Aidha, kuwepo kwa mianya ya uingizaji wa silaha nchini kwa njia haramu kutokana na udhaifu uliopo katika mipaka mipaka ya DR Kongo, Burundi, Rwanda na hata Zambia jambo ambalo ni hatari.    


Posted  Januari4  2014  saa 11:7 AM
Kwa ufupi
  • Mauaji sasa yamefikia tembo 10,950 kwa mwaka 2013, ni dhahiri bila juhudi za kutokomeza ujangili... tutafika mwaka 2020 tukiwa hatuna akiba ya tembo.
Dar es Salaam. Kama Tembo wa Tanzania wangeulizwa kuna jambo gani kubwa hawatalisahau kwa mwaka 2013, bila shaka jibu lingekuwa: “Tuliwindwa, tukauawa sisi na watoto wetu na bado tuna hofu.”
Ingawa tembo ni mnyama mbabe awapo porini, lakini uwezo wake wa kujilinda yeye na jamii yake ulipunguzwa nguvu kwa kiwango kikubwa mwaka 2013, baada ya mauaji ya hazina hiyo ya taifa kuongezeka kwa kiasi kikubwa hata kuisukuma Serikali kuanzisha Operesheni Tokomeza Ujangili.
Utekelezaji wa operesheni hiyo ambao ulilenga kuzuia uwindaji haramu wa wanyama hao na wengine walio katika mbuga na hifadhi za taifa huku taarifa zikionyesha kuwa shehena kubwa ya pembe za ndovu ambayo imekuwa ikikamatwa ndani na nje ya nchi. Ripoti ya operesheni hiyo, ilileta athari kubwa kwa wananchi na mifugo hatua iliyomlazimu Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne waliokuwa wakiisimamia wizara zilizotajwa kuzembea katika kusimamia Opereesheni Tokomeza Ujangili.
Mawaziri hao ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Hata hivyo, akizungumza katika salamu zake za Mwaka Mpya, Rais Kikwete alisema: “Tunakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza. Ni muhimu kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.
Kutokana na kukithiri kwa matukio ya ujangili nchini, Mkataba wa Biashara ya Kimataifa kwa Viumbe vilivyo Hatarini (CITES), uliitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi nane duniani zinazoongoza kwa kufanya biashara ya pembe za ndovu.
Matukio yaliyotikisa
Polisi mjini Zanzibar hawataisahau Novemba 15, 2013, siku waliyopigwa na butwaa baada ya kukamata shehena kubwa ya pembe za ndovu katika Bandari ya Malindi, zikiwa na thamani ya Sh7.4 bilioni.
 Awali mzigo huo ulikuwa umehifadhiwa katika Mtaa wa Darajabovu, mkoa wa Mjini Magharibi, kabla ya kusafirishwa hadi Malindi.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisema kuwa baada ya kukamilika kwa kazi ya kupakua na kuhesabu pembe hizo, walibaini kuwa vilikuwa vipande 1,021 vikiwa na uzito wa kilo 2,915.
Tukio jingine la kufunga mwaka ni lile lililotokea jijini Dar es Salaam, ambalo lilisimamiwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Tarish Maimuna ambapo pembe za ndovu 706 zilikamatwa.
Katika tukio hilo, ambalo lilithibitisha kuuawa kwa tembo 353, raia watatu wa China wakazi wa Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni, walikutwa wakiwa wamehifadhi shehena hiyo nyumbani kwao. Watuhumiwa hao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung.
1Baada ya polisi kuongeza nguvu ya kukamata pembe za ndovu, wasafirishaji waliibuka na mbinu mpya. Agosti 16, 2013 Polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na pembe za ndovu yenye thamani ya Sh18.4 milioni zilizotengenezwa kama bangili tayari kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Pia, haitasahaulika siku polisi jijini Dar es Salaam walipomkamata mkazi wa Mwananyamala, waliyemtilia shaka kisha kumpekuwa na kumkuta akiwa na vipande 16 vya pembe za ndovu  vyenye uzito wa kilo 24.5.
Akizungumzia tukio hilo, Kamishina wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema kuwa mtuhumiwa alinaswa na Polisi saa 9 alasiri maeneo ya Msimbazi Center, Wilayani Kinondoni.
Wafanyabiashara wengine walikamatwa nchi jirani wakijaribu kupeleka pembe hizo katika masoko barani Asia, hata hivyo walikamatwa kabla hawajatimiza malengo yao.
Januari mwaka huu, Gazeti La Daily Mail la Uingereza liliripoti kwamba Serikali ya Kenya imekamata shehena ya vipande 638 vya pembe za ndovu ambavyo ni sawa tembo 320 waliouawa.
Mzigo huo wa tani mbili ulikuwa kwenye kontena la mawe ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.
Huko Ruvuma, Polisi walifanikiwa kumtia mikononi dereva wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, akisafirisha vipande 16 vya pembe za ndovu vyenye uzito wa kilo 18 ambavyo zilikuwa na thamani ya Sh48, 000 milioni.
Akisoma hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni ya mwaka 2013/14, Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alisema pembe za ndovu zenye uzito wa tani 4 kutoka nchini Tanzania na Kenya zimeripotiwa kukamatwa na vyombo vya usalama vya mamlaka ya Jiji la Hong Kong, huku zile zilizoibwa kutoka Tanzania zikiwa na thamani ya zaidi ya Sh2.5 bilioni.
“Pembe za ndovu zilizokamatwa Wilaya ya Biharamulo… zikiwa  kwenye gari iliyosemeka  ya Serikali maeneo ya Mto wa Mbu; watu watatu waliokamatwa Masasi wakisafirisha; haya ni matukio machache tu ambayo yaliweza kuripotiwa na Jeshi la Polisi yanayotoa taswira ya tatizo kubwa la ujangili hapa nchini,” alisema Msigwa.
Msigwa aliongeza kuwa iwapo Tanzania itaendelea na kasi iliyopo ya kuuwa tembo, miaka saba ijayo nchi hiyo itakuwa na historia ya kuwa na akiba ya wanyama hao.
“Ikiwa tafiti za mwenendo wa mauaji ya tembo zikionyesha kukua na kuashiria kwamba mauaji sasa yamefikia temboa 10,950 kwa mwaka huu wa 2013, ni dhahiri bila juhudi za kutokomeza ujangili tutafika mwaka 2020 tukiwa hatuna akiba ya tembo tena,” aliongeza.
Akizungumza na Redio Umoja wa Mataifa, Septemba 2013, Kagasheki alinukuliwa akisema kuwa ongezeko la bei ya pembe za ndovu, umasikini wa wananchi na tamaa ya baadhi ya watu zimechochea kwa kiasi kikubwa ongezeko la ujangili nchini.
Imeandaliwa na Goodluck Eliona


No comments:

Post a Comment