Saturday, December 14, 2013

Wafurahia misaada ya TANAPA

15/12/2013
| Posted by Sitta Tumma |


Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kitawasi kata ya Gorong'a wakiwaeleza waandishi wa habari kutoka mikoa mbalimbali waliotembelea vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Taifa ya Serengeti ,kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili na faida wazipatazo za uhifadhi-picha na Journo Tourism

WANANCHI wa Kata ya Gorong’a na Nyarokoba wilayani Tarime mkoani Mara, wameeleza kufurahishwa na misaada ya kijamii inayotolewa na uongozi wa Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA).
Wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea vijiji vilivyo jirani na hifadhi ya Serengeti, ambao wanashiriki semina ya mafunzo ya ujirani mwema baina ya TANAPA na wananchi, baadhi ya wananchi wa kata hizo walisema miradi hiyo imesaidia kuchochea maendeleo.
Kwa mujibu wa wananchi hao, walisema kuwa TANAPA imefanikiwa kujenga Shule ya Msingi Masurura, Kata ya Nyarokoba huku ujenzi huo uligharimiwa na uongozi wa hifadhi hiyo.
“Tunaushukuru sana uongozi wa TANAPA kwa kutujengea shule hapa Masurura. Hii shule wananchi hatukuchangia chochote na gharama zote zilikuwa kwao,” alisema mkazi wa Masurura, Charles Musapya.
Alisema kuwa shule hiyo inachukua kati ya watoto 500 hadi 600, na kwamba msaada huo umesaidia kuondoa tatizo la watoto kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.
Mkazi huyo alisema kuwa uongozi huo wa TANAPA umesaidia pia kujenga zahanati mwaka 2001 katika Kijiji cha Gibaso, ambapo kulikuwa na boma linalotumiwa kama hospitali na uongozi wa hifadhi hiyo ukamalizia kwa kupaua.
Naye balozi wa eneo hilo, John Kendeka alisema kuwa Tanapa wameweza kujenga vyumba vitatu vya madarasa.
Aliiomba serikali kuendelea kuisaidia zaidi jamii inayoishi maeneo ya vijijini, badala ya kuelekeza misaada mingi mijini kwani kufanya hivyo itazidi kuchochea maendeleo.

No comments:

Post a Comment