Na Mashaka Mgeta
29th December 2013
Ni safari ya takribani mwezi mmoja,
ikinifikisha kwenye hifadhi za Tarangire, Kilimanjaro (Kinapa) na Serengeti
(Senapa) ambazo zote zipo chini ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Lakini katika kupata taarifa kwa
upana zaidi kuhusu uhifadhi na utalii wa ndani, ninapanua wigo wa vyanzo
na kufika kwenye pori la akiba la Selou ambapo ninakutana na jamii zinazoishi
kuzizunguka rasilimali hizo.
Yapo mafanikio kadhaa ya kijamii
yanayotokana na uwekezaji wa mamlaka zinazoongoza maliasili hizo, kwa
kugharamia huduma kadhaa za jamii ikiwa ni sehemu ya kuzifanya (jamii hizo)
zinufaike na uwapo wa rasilimali hizo kwenye maeneo yao.
Kwa maana nyingine, kunufaika
kunakotokana na uwapo wa maliasili hizo kunazifanya jamii zinazoishi maeneo
yanayozizunguka, kuhisi umiliki wake na hivyo kuzilinda na kuziendeleza.
Miongoni mwa maeneo yanayozizunguka
maliasili hizo kumefanyika ujenzi ama ukarabati wa nyumba ama ofisi zilizo
katika sekta za afya, elimu na nyinginezo.
Mary Safari ni Mjumbe wa Kamati ya
Mazingira na Uhifadhi ya kijiji cha Mamire wilayani Babati mkoa wa Manyara,
kikiwa ni miongoni mwa maeneo jirani ya hifadhi ya Tarangire.
Anasema katika kipindi cha maisha ya
zaidi ya miaka 34 akiwa kijijini hapo, hakuwahi kuwaona ‘uso kwa uso’ baadhi ya
wanyamapori, zaidi ya kuwashuhudia kwenye picha za video.
Hata hivyo, anasema mapema mwaka huu,
uongozi wa hifadhi ya Tarangire uliwaalika viongozi wa kata ya Mamire na yeye
(Mary) akitokea kijiji cha Mamire, alishiriki ziara hiyo.
“Tulipoingia hifadhini nilishangaa
kuwaona wanyama ambao sikuwahi kuwaona kabla na wengine nilikuwa ninawashuhudia
kwenye picha za video,” anasema.
Mary ambaye ni mama wa watoto watatu,
anasema baada ya ziara iliyofanyika Tarangire, amekuwa miongoni mwa watetezi wa
uhifadhi na utangazaji wa utalii wa ndani.
“Zamani nilikuwa nafuata mkumbo kwa
kuamini kwamba hifadhi kama ya Tarangire na wanyamapori waliomo ni adui zetu,
lakini sasa hivi nipo mstari wa mbele kuzitetea,” anasema.
Anaongeza, “jamii ikishirikishwa kwa
kina kuujua undani wa manufaa ya hifadhi ama mapori ya akiba tunayoishi karibu nayo,
ni dhahiri kwamba kutakuwa na mabalozi wengi wa uhifadhi na utangazaji wa
utalii wa ndani.”
Mary anasema ni ukweli usiopingika
kwamba jamii zinazoishi karibu na hifadhi ama mapori ya akiba, zimekuwa
zikiathirika kutokana na kuvamiwa na wanyamapori pori wanaoharibu mali hasa
mazao yao.
“Utakuta mtu anamiliki eneo dogo
lenye mazao ambayo yakiharibiwa na mnyamapori, basi hilo linakuwa jambo la
uadui mkubwa,” anasema.
Si Mary pake yake, bali wananchi
kadhaa wanaozizunguka hifadhi na mapori ya akiba, wanaielezea hali hiyo kuwa
inachochea dhana kwamba hifadhi na wanyamapori ni adui wa binadamu.
Lakini Mary anasema pamoja na
uhalisia huo, ushirikishwaji umma katika masuala ya hifadhi kunaweza kuwafanya
watu wakatoa ushirikiano wa kutosha kwa maofisa wa wanyamapori ili kudhibiti
uharibifu unaotokana na wanyama hao.
Anasema hata inapotokea kuwapo
ushirikishwaji huo, jamii zinazozizunguka hifadhi na mapori ya akiba,
zitajiepusha na vitendo vya uharibifu badala yake kuendeleza uhifadhi, kwa vile
wanatambua umuhimu wake kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.
Mary anasema hali hiyo imedhihirika
kwake binafsi ambapo sasa, anazungumzia umuhimu wa Tarangire katika hafla
zinazofanyika ndani na nje ya wilaya ya Babati, kisha kuwashawishi watu
kuitembelea.
Afisa Mtendaji wa kijiji cha Mamire,
Juma Jumbe, anaungana na hoja za Mary, akisema uongozi wake uliotambua
umuhimu wa kuishirikisha jamii hiyo iujue umuhimu wa Tarangire, hivyo kuwa
mabalozi wa uhifadhi na kuutangaza utalii wa ndani.
Jumbe, anasema walipata mwaliko wa
watu 18 wanaotoka kwenye maeneo yanayozunguka Tarangire, kwenda kuitembelea
hifadhi hiyo ikiwa ni sehemu ya kukuza ujirani mwema unaochochea uhifadhi na
utalii wa ndani.
Walisema waliokuwamo kwenye ziara
hiyo ni pamoja na wawakilishi wa vyama vya kimila, wazee, viongozi wa umma na
dini na wajumbe wa kamati ya mazingira.
Jumbe anatoa mfano kuwa
kutoishirikisha jamii katika kiwango kizuri kwenye uhifadhi wa Ziwa Babati
lililo miongoni mwa vivutio vya utalii, kumeliweka katika hatari ya kutoweka.
“Si rahisi kuzungumzia uhifadhi na
utalii wa ndani kama jamii zinazozunguka hifadhi na mapori ya akiba,
hazitashirikishwa badala yake maliasili hizi zionekane kuwapo kwa ajili ya
wageni kutoka nje hasa wazungu,” anasema.
Jumbe anasema kabla ya kuboreshwa kwa
mpango wa ujirani mwema kati ya Tarangire na jamii zinazoishi kuizunguka,
palikuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira na uuaji wa wanyamapori.
“Pamoja na changamoto zilizojitokeza
hivi karibuni, lakini sasa hivi kuna mwamko unaoiwezesha jamii kuendeleza
uhifadhi na kutangaza utalii wa ndani,” anasema.
Hassan Limbega ni Afisa Ardhi na
Maliasili katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, anasema ushiriki wa jamii zinazolizunguka
pori la akiba la Selou, umekuwa nyenzo muhimu katika uhifadhi wake.
Limbega, anasema ushiriki huo
umeiwezesha jamii kutambua mambo ya msingi yakiwamo ya kisheria kama vile
ilivyo kosa kuua mnyamapori.
“Baada ya kuwashirikisha wananchi sasa
wamekuwa wasaidizi wa karibu wa idara yetu katika kukabiliana na changamoto za
uhifadhi na kuwadhibiti wanyama wanaoharibu mali zao,” anasema.
Anasema, tofauti na ilivyokuwa awali,
hivi sasa anapotokea mnyamapori kuingia eneo la makazi na kuharibu mali
yakiwamo mazao, jamii zinazoishi pembezoni mwa Selou hazimuui, bali kuwasiliana
na askari wa wanyamapori.
Limbega, anasema zaidi ya uhifadhi
jamii hizo zinasaidia pia udhibiti wa ujangili hasa wa wanyamapori wadogo
wanaowindwa na walio miongoni mwao.
Kwa mujibu wa Limbega, mpango wa
ushirikishi wa jamii zinazoizunguka Selou wilayani humo, umefanikisha kuundwa
kwa askari wa hifadhi kwenye ngazi za vijiji, wakiwa wanasimamiwa na asasi za
kiraia (CBOs).
Hata hivyo, Limbega anapendekeza
kwamba katika kukuza utalii wa ndani, ipo haja ya kutangaza vivutio vingine
visivyojulikana, vikiwamo vinavyopatikana kuzunguka hifadhi na mapori ya akiba.
Pia anasema kwa vile uhifadhi na
utalii wa ndani unahitaji rasilimali watu na fedha, ipo haja kwa mamlaka husika
kufikiria namna bora ya kuziongeza ili zikidhi mahitaji kwa maeneo husika.
Meneja Uhusiano wa Hifadhi za Taifa
(Tanapa), Paschal Shelutete, anasema uwekezaji katika kuboresha huduma za
jamii, ni moja ya ajenda zenye kipaumbele kwa mamlaka hiyo.
Shelutete, akizungumza ofisini kwake
mjini Arusha, anasema mbali na kuwekeza katika huduma hizo, Tanapa kama ilivyo
kwa mamlaka za maliasili nyingine, imekuwa ikisaidia shughuli za kijamii
hususani kupitia asasi za kiraia zilizo kwenye sekta za umma na binafsi.
Hali hiyo inastahili kuwa miongoni
mwa mafanikio yenye taswira chanya katika uhifadhi na uenezi (utangazaji) wa
utalii kwa raia wa ndani.
Ingawa ni hivyo, yapo maeneo kadhaa
ambayo yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili azma ya uhifadhi na utangazaji wa utalii
wa ndani, viwe endelevu kwa maslahi ya nchi na watu wake.
Kwa hali ilivyo sasa, wananchi
wanaoishi maeneo ya kuzizunguka hifadhi za taifa, mamlaka za uhifadhi na mapori
ya akiba, wanatoa ushauri unaolenga kuongeza kiwango cha ushiriki wao kwenye
uhifadhi na utangazaji wa utalii wa ndani.
Tanzania kupitia taasisi zilizopo
chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, hususani Tanapa, imekuwa mstari wa
mbele kuhakikisha jitihada kadha wa kadha zinafanyika katika kuendeleza
uhifadhi na kutangaza utalii wa ndani.
Sekta ya utalii imekuwa moja ya
vyanzo vya mapato, na kutokana na takwimu za mwaka jana zilizotolewa na
aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ulichangia
asilimia 17 ya pato ya taifa.
Ingawa ni hivyo, takwimu zinaonyesha
kwamba idadi ya Watanzania wanaoshiriki utalii wa ndani ni ndogo ikilinganishwa
na wanaotoka nje ya nchi, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili
kuondokana na kasoro hiyo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment