Na Moshi Lusonzo
29th December 2013
Kaimu kamanda wa kikosi cha polisi
cha Tazara, (SSP) Inocent Mgaya (katikati) akiwa na OCD wa kituo hicho SP,
Bakari Makuka (kushoto) na SP, Shaaban Hussein wakionesha meno ya tembo kwa
waandishi wa habari.
Meno ya tembo yenye thamani ya Sh.
milioni 25.5 yamekamatwa ndani ya treni ya Tazara katika stesheni ya Kisaki,
Wilaya ya Morogoro Vijijini, yakisafirishwa kuelekea jijini Dar es
Salaam.
Meno hayo yalikamatwa Alhamisi wiki
hii, ikiwa ni siku chache baada ya mawaziri wanne kuondolewa madarakani
kutokana na kutosimamia vizuri zoezi la 'Operesheni tokomeza majangili '.
Akizungumza jana, Kaimu kamanda wa
kikosi cha polisi cha Tazara, (SSP) Inocent Mgaya, alisema katika tukio hilo
alikamatwa Ally Juma (26), maarufu Ngagari, fundi seremala na mkazi wa
Kisaki.
Kamanda Mgaya, alisema walipata
taarifa kutoka kwa raia mwema kuwa kuna mtu amebeba meno ya tembo ndani ya
treni hiyo iliyokuwa ikitokea Zambia kwenda jijini Dar es Salaam.
Alisema baada ya kufanya upekuzi
katika behewa namba M2, walifanikiwa kumkamata mtu huyo akiwa na mabegi mawili
yakiwa yamehifadhiwa pembe 14 za tembo na kipande kimoja cha jino la kiboko.
"Tulipomkamata na kumfanyia
upekuzi tuligundua begi la kwanza lilikuwa na vipande vinane vya pembe nane na
la pili aliweka vipande saba," alisema Kamanda Mgaya.
Alisema kwa kushirikiana na wataalamu
kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, walibaini vipande hivyo vya pembe za
tembo vina uzito wa kilo 29 vyenye thamani ya Dola za Kimarekani 1950
(Sh. 25,520,000).
Jino la kiboko lilikutwa na uzito wa
gramu 900 lenye thamani ya Sh. milioni 2.5.
"Nataka kuweka wazi kwamba
usafiri wa treni ni kwa ajili ya watu kupata usafiri wa uhakika na sio
vinginevyo, polisi wapo makini kuhakikisha hakuna mtu anayetumia chombo
hiki kwa uhalifu," alisema.
Aidha, kwenye tukio hilo polisi
walikamata mifuko miwili ikiwa imepakiwa madawa ya kulevya aina ya bangi.
Hata hivyo, hakuna mtu aliyekamatwa
kuhisika na mifuko hiyo yenye uzito wa kilo 19.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Habari Zaidi
No comments:
Post a Comment