Thursday, December 19, 2013
Tanzania yang’ara utalii Afrika
TANZANIA imeng’ara katika sekta ya utalii barani Afrika baada ya kuwa nchi ya kwanza kwa kuvutia zaidi watalii huku hifadhi za Serengeti na Ruaha zikiongoza kwa ubora wa utalii.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), aliyasema hayo juzi wakati akifunga mafunzo ya mwezi mmoja kwa askari 20 wa utalii wa miguu katika hifadhi za Ruaha, Mikumi na Udzungwa yaliyofanyika katika hifadhi ya taifa ya Ruaha, Iringa.
Dk. Dembe alisema kuwa Tanzania imeonekana ni nchi ya kwanza kwa utalii baada ya wataalamu wa masuala ya utalii barani humo kuchagua nchi nane bora kwa safari za utalii.
Alizitaja nchi zilizoshindanishwa na Tanzania kwa kupigiwa kura kuwa ni Botswana, Uganda, Namibia, Afrika Kusini, Kenya, Zambia na Zimbabwe.
Alisema mbali ya kuchagua nchi inayofaa kwa utalii, pia walitazama maeneo 50 yaliyofaa kwa safari za utalii, na Tanzania ikifanikiwa kupata maeneo kumi bora, zikiwemo hifadhi nane, huku Mlima Kilimanjaro ukikosekana kwa vile ni maalumu kwa kupanda tu.
Dk. Dembe alisema hivi sasa Tanapa wameelekeza nguvu zote katika kuendelea kuitangaza hifadhi ya Ruaha ikiwa ni pamoja na kubadilisha mazingira yake ili kuvutia idadi kubwa ya watalii. Hifadhi hiyo ndiyo kubwa kuliko zote Tanzania.
Hata hivyo, alisema kuwa katika kuboresha utalii wa kusini, Tanapa ipo katika mkakati wa kutoa elimu kwa madereva wanaopeleka wageni hifadhi mbalimbali ili kuepuka udereva wa vurugu.
Alisema kuwa utalii ni sekta nyeti katika taifa, hivyo lazima wale wote wanaohusika wawe na elimu ya kutosha juu ya utalii na kuyataka makampuni kuepuka kuwatumia madereva wa daladala kupeleka wageni hifadhini.
Aliwataka askari hao kuwa wazalendo na kuepuka kuwa maadui wa hifadhi kwa kushirikiana na majangili kuzihujumu.
Wakati huo huo, Dk. Gembe alivitaka vyombo vya habari na wanahabari nchini kuendelea kutangaza utalii ikiwa ni pamoja na kuepuka kuandika habari ambazo hazisaidii katika ukuzaji wa sekta hiyo.
Alisema iwapo vyombo vya habari nchini vitafanya vizuri katika kuhamasisha utalii na kuepuka kuandika habari za kutisha wageni kufika katika hifadhi, ni wazi sekta hiyo nchini itakua.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment