16/12/2013 | Posted by Dixon Busagaga | Kilimanjaro
SERIKALI
imekumbushwa kutekeleza ahadi yake ya kuwadhamini watu 100 wakiwamo askari wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kupanda Mlima Kilimanjaro kama sehemu ya
maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Uhuru wa Tanganyika.
Ahadi
hiyo ilitolewa mwaka jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kagasheki,
katika maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika ambapo pia alipokea timu
ya watu 32 waliokuwa wamepanda mlima huo wakiwemo wabunge walio kwenye Kamati
ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Akikumbushia
ahadi hiyo, Meja Jenerali Mstaafu, Christopher Gimonge, alielezea kutopendezwa
na utekelezaji wa ahadi hiyo ambapo kwa mwaka huu vijana watano pekee kutoka
JWTZ ndio walioshiriki zoezi la kupanda Mlima Kilimanjaro linalofahamika kama
Uhuru Expedition.
Naye
aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jenerali Mstaafu George
Waitara, aliishauri serikali kuunda vitengo maalumu katika wizara mbalimbali
kwa ajili ya ufuatiliaji wa ahadi za mawaziri, ili kulinda heshima ya serikali
mbele ya jamii.
Waitara
ambaye ndiye kiongozi na msimamizi mkuu wa zoezi hilo kila mwaka ameihakikishia
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa jeshi hilo litaendelea kuunga mkono juhudi
za TTB katika kuvitangaza vivuto vya utalii vya Tanzania ukiwemo Mlima
Kilimanjaro.
“Licha ya
changamoto zinazojitokeza bado jeshi la wananchi litaendelea kushiriki katika
kutangaza vivutio vya utalii hasa Mlima Kilimanjaro kupitia msafara wetu kwa
kuupanda mlima huo kila mwaka maarufu kama Uhuru Expedition ikiwa ni sehemu ya
kuadhimisha Uhuru wa
Tanzania,” alisema Waitara.
Tanzania,” alisema Waitara.
Mkuu huyo
wa jeshi la ulinzi mstaafu aliishukuru pia hifadhi ya taifa ya Mlima
Kilimanjaro (Kinapa) kwa msaada ambao imekuwa ikitoa kwa msafara huo na
kuwezesha wapandaji kutimiza azma yao ya kuutangaza mlima huo mrefu kuliko yote
barani Afrika.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB, Balozi Charles Sanga, aliyeshiriki kupanda mlima
huo mwaka huu alisema Bodi ya Utalii inayo furaha kuona Uhuru Expedition
iliyoasisiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania inaendelea kuimarika na
kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake.
No comments:
Post a Comment