Makala
Toleo la 325
Raia Mwema
13 Nov
2013
- Balozi
Kagasheki aachwe achape kazi
KATIKA kipindi cha miaka mitatu iliyopita kumekuwa
na kelele nyingi kutoka kwa wabunge, wanaharakati, vyombo vya habari na
wananchi wa kulaani mauaji ya tembo. Mbali na kuulani huko, wamekuwa wakiilaumu
serikali kwa kutokuchukua hatua muafaka kumaliza tatizo hili.
Wengine wamedai hali ni mbaya, wakitaka sheria
itungwe ili majangili wapigwe risasi, wapo waliotaka waziri mwenye dhamana
ajiuzulu huku wengine wakilalamika na kutaka tumwachie Mungu!
Ni kweli hali ya ujangili dhidi ya tembo nchini
imekithiri na hakuna mbadala zaidi ya kuchukua hatua muafaka. Waziri mwenye
dhamana, Balozi Khamisi Kagasheki, akiweka wazi hili katika Bunge la bajeti
lililopita alihadharisha kuwa inaandaliwa operesheni maalumu.
Kwamba ‘Operesheni Uhai’ iliyofanyika mwishoni mwa
miaka ya 1980 ingekuwa ndogo kulinganisha na hiyo iliyokuwa ikiandaliwa.
Katika utatuzi wa tatizo lolote kuna mbinu kuu
tatu. Mbinu za kawaida ambazo ni endelevu (proactive), mbinu zinazolenga kuzuia
tatizo (preventive au deterrent) na mbinu za kujibu mapigo (reactive).
Wakati mbinu mbili za kwanza zinatoa muda mrefu wa
kujipanga na aghalabu huwa shirikishi, mbinu ya tatu ni ya haraka na inachukua
sura ya udharura na pengine haitoi fursa kwa demokrasia.
Kwa mfano, kinapozuka kipindupindu mahali au nyumba
inapoungua huwezi kuahirisha hatua ili kungoja ridhaa ya kikao au kuandaa
semina kuelimisha watu namna ya kukabili tatizo.
Ni kweli kwamba mbinu mbili zilizotajwa hapo juu
(proactive na preventive) zimekuwa zinatumiwa na mamlaka husika kupambana na
tatizo la mauaji ya tembo. Hata hivyo, sababu kadhaa zimegeuza ujangili wa
tembo kuwa janga na hivyo kufanya njia hizi mbili zisiwe ‘toshelevu’.
Tembo wengi wanauawa kutokana na kukua kwa soko
katika nchi za mashariki ya mbali. Aidha, ongezeko la wageni kutoka katika nchi
hizi; ongezeko la wahamiaji haramu na urahisi wa wahalifu kupata silaha za
kivita; kushuka kwa maadili na uzalendo miongoni mwa Watanzania watumishi na
wasio watumishi; kuimarika kwa miundombinu (barabara) na njia za mawasiliano
(simu za mikononi) na jiografia yetu (kupakana na Bahari ya Hindi) ni mambo
yanayochangia ongezeko la mauaji ya tembo na biashara haramu ya meno yake.
Katika hali ambayo tembo wengi wanakufa kila siku
kiasi cha kutishia uwepo wake katika miaka michache ijayo, hakuna njia nyingine
yoyote ya kukabili tatizo hili zaidi ya kuchukua hatua za dharura na haraka
(reactive measures). Na hili ndilo lililofanywa na serikali kupitia kwa waziri
mwenye dhamana ambaye alitangaza ‘Operesheni Tokomeza’.
Naamini hatua hii ni ya kupongezwa. Waziri
Kagasheki amethubutu na nina hakika akisaidiwa na kuungwa mkono ataweza. Kuna
wanaodai operesheni hii si suluhisho. Kwa bahati mbaya Watanzania tumekuwa
wepesi kukosoa bila kutoa suluhisho mbadala. Ni vema wale wanaokosoa
wakatuambia dawa mujarabu ya kumaliza tatizo hili ni ipi.
Wakati matunda ya operesheni hii yameanza
kuonekana, inashangaza wanapojitokeza wanasiasa na ‘wanaojiita wanaharakati’
kumshambulia waziri ambaye wengi wanaomfahamu hawajawahi kutilia shaka uadilifu
na utendaji wake kwa umma.
Kimsingi, wanasiasa na wanaharakati hawajamtendea
haki Kagasheki, hawajazitendea haki maliasili zetu na hawajaitendea haki nchi
hii. Ninachokiona hapa ni baadhi ya wanasiasa kutumia mbinu chafu kujijenga
kisiasa. Lakini pia kuna uwezekano kuwa wapinzani wa vita hii wana maslahi
kutokana na wao binafsi au jamaa zao kuhusika katika dhambi hii kubwa ya
kuangamiza tembo.
Ama nyingi ya asasi (NGOs) zinazodai kutetea haki
za binadamu inaeleweka kuwa nyingi zipo, si kwa maslahi hasa ya Watanzania,
lakini ni mashine za watu za kuvuna pesa. Asasi hizi, mara nyingi zimekuwa
zikiunda hoja hasi dhidi ya serikali ili kujenga uhalali wa kupata pesa kutoka
kwa wafadhili wao na ndio maana watendaji wake wana utajiri wa kutisha.
Wangekuwa wakweli wangeonesha pia kusikitishwa na
vifo vya askari waliokufa kwa kuuawa na majangili. Inakuwaje mtu kulalamikia
ng’ombe kukamatwa ndani ya hifadhi lakini asiguswe na vifo vya binadamu
vinavyosababishwa na majangili? Huo uzalendo uko wapi? Ni vema asasi hizi
zikaendelea kuwepo na kutengeneza pesa, lakini si kwa mbinu chafu kama hizo.
Kauli ya mbunge mmoja kuwa eti “..watu waliokamatwa
ndani ya hifadhi wamepigwa na kuumizwa wakati majangili wa tembo wameachwa” si
kwamba tu inakatisha tamaa, bali pia inaonesha ni aina gani ya wabunge tulinao.
Mbunge angewasaidia Watanzania kama angetuambia
waliokamatwa ndani ya hifadhi walifuata nini na kwa sheria gani. Aidha,
alitakiwa kutusaidia kuwa majangili wa tembo wanaohusika ni kina nani hasa!
Ieleweke kuwa hii vita si ya Kagasheki peke yake.
Hivyo hao wanaowajua majangili wamsaidie ili sheria
ichukue mkondo wake. Sasa mbunge aliyekula kiapo cha kuilinda katiba na
kutumikia umma anapojua wahujumu kama hao halafu akakaa kimya mpaka Kagasheki
aje awajue, anatoa matumaini gani kwa Watanzania?
Kwa tafsiri yangu, mbunge wa namna hii ni msaliti
wa nchi yetu. Mwingine, tena waziri analalamikia msaidizi wake kukamatwa. Hivi
msaidizi wako akituhumiwa kwa uhalifu ana kinga gani ya kutokukamatwa na
kuhojiwa?
Operesheni yoyote ile duniani kote inapotokea huwa
kuna kasoro za hapa na pale. Hata nchi zilizoendelea zimejikuta zikifanya
makosa katika operesheni kama hizi na pengine hata kusababisha watu wake
kupoteza maisha (rejea Marekani na vita ya magaidi).
Lakini pia hata kwenye sayansi za tiba karibu dawa
zote huwa na madhara ya kando (side effects) lakini baadaye hupatikana tiba ya
kudumu. Labda wanasiasa na wanaharakati wetu wangetusaidia sana kama wangetupa
mfano wa operesheni yoyote ile ambayo haikuwahi kuwa na kasoro.
Hata hivyo, kama wote tunakubali kuwa mapambano
dhidi ya ujangili wa tembo ni vita ya lazima, hivi kukijitokeza kasoro unaamua
kuachana na hiyo vita? Inapotokea unasafiri kwa gari ikapata pancha, unaamua
kuachana na safari na kumfukuza dereva?
Binafsi sitaki kuamini wale wanaomshambulia Waziri
Kagasheki wana uchungu na nia ya dhati na maisha ya Watanzania wenzao.
Ninachoamini ni kwamba kuna ajenda iliyojificha. Nashawishika kuamini hivyo kwa
kuwa ni wabunge hawa hawa waliokuwa wanapiga kelele kwamba tembo wanakwisha,
sasa wamemgeuka Balozi Kagasheki.
Leo Balozi Kagasheki anapofanya kweli wabunge hao
hao wanadai ajiuzulu kwa kuvunja haki za binadamu! Hivi huu unafiki wa wabunge
wetu utaisha lini? Hivi maslahi gani ya nchi wanayopigania?
Pale Kagasheki alipotangaza kusitisha ‘Operesheni
Tokomeza’ (tangazo ambalo nahisi pengine hata yeye hakulifanya kwa ridhaa
yake), sikutarajia wabunge wangekubaliana nalo. Cha ajabu, wengi waliochangia
tamko hili la wizara walijielekeza kwenye lawama dhidi yake na wahusika wengine
kwenye operesheni hii na kuonyesha kuguswa kwa masikitiko na kitendo cha
ng’ombe pamoja na watu kukamatwa.
Katika michango yote, wabunge wengi wakiwemo wale
wanaopenda kujipambanua kama wazalendo hawakuonyesha kukerwa na mauaji ya
tembo! Hili linazua maswali. Je, kelele zote walizokuwa wakipiga dhidi ya
ujangili zililenga kukejeli wananchi kwamba wana uchungu na rasilimali za
taifa?
Je, katika hali kama hii ambapo wanaonyesha wazi
kupinga operesheni, ni kitu gani kitasababisha tusiwaunganishe na mtandao wa
ujangili? Je, kwa nini tusiamini kuwa lawama zote na chuki zinazoelekezwa kwa
Balozi Kagasheki zimejificha kwenye maslahi ya kisiasa zaidi?
Nawasihi Watanzania wote wenye nia njema na hatima
ya maliasili zetu kuendelea kuunga mkono kwa nguvu zote juhudi za kupambana
dhidi ya janga la ujangili wa tembo na rasilimali nyingine za taifa. Tuwe
makini na wanasiasa wanafiki wanaotumia shida, misiba na majanga yetu
kujinufaisha kisiasa.
Namsihi Waziri Kagasheki na watendaji wengine wote
wenye mtazamo chanya kwa taifa letu wasikatishwe tamaa. Ieleweke kuwa, katika
hali ambayo watu wameingia kwenye siasa kwa mbinu chafu, si rahisi kwa watu
waadilifu, makini na wenye viwango vya hali ya juu vya utendaji kama Balozi
Kagasheki kukubalika.
Watapigwa vita na kuchafuliwa bila sababu za
msingi. Imani kubwa iko kwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye ndiye aliyempa dhamana
Waziri Kagasheki.
Hotuba yake aliyotoa bungeni, inatoa matumaini
kwamba fitna na chuki zinazoelekezwa kwa Balozi Kagasheki na wasioitakia mema
nchi yetu kwa kivuli cha uzalendo na kutetea haki za binadamu zitashindwa.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mwandishi
wa makala hii anaitwa Elifuraha Mchangila
No comments:
Post a Comment