Thursday, November 14, 2013

Ujirani mbovu chanzo cha moto Mlima Kilimanjaro


Rodrick Mushi-Tanzania daima

MLIMA Kilimanjaro umelijengea heshima kubwa taifa la Tanzania ukiachilia mbali mapato yanayopatikana kutokana na wageni wanaofika kupanda mlima huo.
Mlima huu ambao una urefu wa mita 5,895 (futi 19,340) unachangia zaidi ya asilimia 40 ya pato la taifa, huku kila mwaka mapato yanayotokana na utalii wa Mlima Kilimanjaro ni zaidi ya sh bilioni 80.
Licha ya mapato makubwa yanayotokana na mlima na fursa ya ajira, kuna hatari ya kutoweka kwa mlima huo, kutokana na theluji ya mlima kuendelea kupungua na kuwapo kwa moto ambao umekuwa ukiwaka na kuchoma misitu ya asili karibu kila mwaka.
Ripoti mbalimbali za tafiti juu ya hali ya Mlima Kilimanjaro zimekuwa zikifanywa na kueleza hali mbaya ya mlima hususan theluji ya mlima kutoweka.
Mmoja wa watafiti, Jacques Blot wa Chuo Kikuu cha Bordeaux, Ufaransa kwenye moja ya tafiti zake anasema tangu mwaka 1912 theluji ya mlima imepungua kwa zaidi ya asilimia 80.
Ripoti nyingine zinaeleza kuwa theluji ya  mlima ilikuwa kwenye maeneo sita yenye barafu lakini sasa ni maeneo matatu pekee yaliyobaki.
Licha ya kuwapo kwa sababu za asili ambazo zimechangia kupungua huko lakini pia kuna sababu nyingine zinazotokana na uzembe wa kiutendaji wa viongozi wetu.
Ilikuwa Julai 7, mwaka huu nilipopokea simu ya mwananchi mwenye uchungu na nchi hii akisema eneo la kaskazini mwa Mandara katika Mlima Kilimanjaro moto mkubwa unawaka.
Eneo lenye ukubwa wa ekari 40,000 liliteketea kwa moto.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Mahusiano na Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Pascal Shelutete, anasema kuibuka kwa moto huo si mara ya kwanza kwani mwaka 2009 eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 70,000 pia ziliteketea kwa moto.
Tangu miaka ya 1960 Mlima Kilimanjaro umekuwa ukiwaka moto, lakini licha ya madhara yake kwa miaka hiyo, si kama ilivyo sasa, ambapo kuna uhaba wa mvua na unyevu, hivyo lazima madhara yawe makubwa.
Mlima Kilimanjaro unaozungukwa na halmashauri za wilaya sita; Siha, Hai, Moshi Vijijini, Moshi Mjini, Rombo na Same, licha ya kuzalisha mapato mengi lakini wananchi wanaouzunguka mlima huu hawanufaiki, wengi wao ni maskini.
Lakini viongozi wa hifadhi wamebaki kushikilia kuwa mahusiano ni mazuri na wanaendelea kuimarisha mahusiano huku mambo wanayozungumza yakiwa kwenye maneno na maandishi lakini wananchi hawanufaiki kwa lolote.
Wananchi hawaoni faida yoyote ya kuwa karibu na mlima, wengine wanadiriki hata kutosaidia shughuli za kuzima moto, hivyo utaona ni jinsi gani itakuwa vigumu kwa hifadhi kuendelea kubaki salama na kupambana na vitendo vya uharibifu wa mlima.
Mlima Kilimanjaro una eneo kubwa na msitu mnene; ni dhahiri kuwa kwa kutokuimarishwa kwa ujirani mwema lazima vitendo hivi vya moto vitaendelea na hatimaye mlima huu barafu itakwisha pamoja na uoto wa asili na kubaki jangwa.
Tatizo jingine ni kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya majirani wa mlima na askari ambao wamepewa jukumu la kulinda mlima huo.
Najua Tanapa wanatekeleza wajibu wao ila kwenye vijiji vingi nilivyopata fursa ya kutembelea kuna umuhimu wa kuwachukulia hatua askari ambao wamekuwa wakilalamikiwa kuwafanyia wananchi vitendo ambavyo si vya kibinadamu wanapowakuta wameingia kwenye hifadhi.
Hushangai kukutana na mwananchi, tena mwanamke akakuambia amekutwa na askari wa Hifadhi ya Kilimanjaro (Kinapa) akikata majani akalazimishwa ale majani.
Sisemi wananchi wavunje sheria zilizopo, la hasha! Ila sheria ichukue mkondo wake, hata kama mtu amevunja sheria pia ana haki ya kuwajibishwa kwa kutumia sheria aliyoivunja na si kumuwajibisha utakavyojisikia.
Kinapa ijitazame upya katika hili, kwani vitendo hivyo vikiendelea vya ukatili kwa wananchi ambao ndio wanaoishi karibu na mlima kuliko askari wachache ni dhahiri kuwa lazima vitendo vya uharibifu vitaendelea.
Kwanini hatuwezi kujiuliza ni kwanini tangu tunapata taarifa za moto haujawahi kuwahiwa kuzimwa bila kuteketeza ekari nyingi?
Tanzania yetu tunaijua na viongozi wetu tunawajua, wakizungumza ni kama malaika, lakini matendo yao hayaendani na wanachozungumza, hivyo ni vema Kinapa ikaimarisha mahusiano ya ujirani mwema ili wananchi waone faida ya kuwa karibu na mlima kabla ya kuchukua hatua nyingine.
Hivi sasa wizara ndiyo inaona umuhimu wa kuanzisha mfuko wa kuulinda Mlima Kilimanjaro dhidi ya majanga ya moto, yaani utafikiri moto umeanza mwaka huu, ambapo tunarudi palepale kwa niliyoyazungumza, kwani mpango huo utategemea wananchi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi, ambao wametelekezwa na hawaoni faida ya kuwa karibu na hifadhi, hivi kweli tutafanikiwa? Tunapaswa kujiuliza.


No comments:

Post a Comment