Saturday, November 2, 2013

Ujangili ukiendelea kuchekewa utamaliza wanyama

                         Munubhi Munubhi


WAZO binafsi ni kuamini kuwa kama kuna utatu mtakatifu, mfano wa ule wa mbinguni, basi utatu huo mtakatifu kwetu Tanzania ni Ikulu, Mahakama na Bunge tukufu, mahali ambapo hakika panasimamia na kuwakilisha mamlaka, haki na usawa ili kudumisha amani nchini.

Wakati tukiwa na taasisi hizo ‘takatifu’ hususan Bunge, tena moja, lenye wajibu muhimu wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa wananchi kumezuka minong’ono kwamba baadhi ya wawakilishi wetu hao wamegeuka kuwa ‘watetezi’ wa watuhumiwa mbalimbali likiwamo hili la ujangili tena ndani ya chombo cha kutunga sheria!

Zipo taarifa mbalimbali zinazonukuliwa na vyombo vya habari kama vile: ‘Ujangili kulitesa Bunge’ na kadhalika; na wabunge kukinzana vikali huku suala la ujangili likifahamika wazi wazi miongoni mwa Watanzania kuwa ni moja ya tuhuma za makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria zetu hizo hizo zilizotungwa na kupitishwa na Bunge letu.

Kama hivi ndivyo, ni kwa vipi sasa katika suala hili la ujangili ambalo ni tuhuma nzito ya uhalifu linazusha kuwepo kwa pande mbili kinzani bungeni, moja ikiwa mtetezi mkuu na kwa kauli za hisia kali hasa baada ya upande mwingine kutoa taarifa na hata ushahidi wa awali kwa wahusika wanaojihusisha wakiwamo wale walionaswa.

Wazo jepesi na mtazamo wangu ni kuwa hawa ‘watetezi’ wanaotumia kauli kubwa, nzito na za hisia kali kuwatetea hata baadhi ya watuhumiwa walionaswa na vyombo vingine vya dola katika ujangili hakika hawawatendei haki Watanzania na vyombo vingine husika vya dola na wala utetezi huo haujengwi kwa kuzingatia msingi wa utawala bora, kwani zipo mahakama ambapo ni mahali mahususi kwa utetezi  kama huo kwa wahusika.

Pasipo shaka utetezi kama huo ambao huenda hauzingatii misingi ya utawala bora, yaani wa kuzingatia mifumo ya sheria unaweza kutengeneza na kuzusha hisia miongoni mwetu wananchi tunaowakilishwa kwamba pengine watetezi hao wana masilahi binafsi katika suala la ujangili na si bure.

Kwa mantiki hiyo, ndiyo sababu kwa sasa kuna kushutumiana kwa hali ya juu kuhusu majangili ni kina nani, wakati wanajulikana na hata kufikia hatua ya kuomba kutajana kwa majina kwa wahusika humo humo bungeni.

Lililo dhahiri na la kujiuliza ni kuwa: Je, ni kweli  kwamba uhalifu wa ujangili umepiga hodi bungeni kwa baadhi ya wabunge kujihusisha na uhalifu huo tena kwa kutumia kofia za heshima na utukufu wa Bunge letu?

Hapa sinuii kamwe kusema kuwa waheshimiwa wabunge au baadhi yao wanajihusisha na uhalifu wa ujangili nchini, la hasha, lakini kinachosemwa na wao wanachosema, wakiwa pia ni wananchi wana ndugu na marafiki zao ambao kuwatetea hao juu ya ujangili kunazusha shaka kuwa utetezi huo si bure, bali huenda ni utetezi wa kimasilahi.

Ndiyo sababu habari zinazonukuliwa na vyombo vya habari ambazo hazijakanushwa pia zinasema: ‘Ujangili kulitesa Bunge’, ndipo najiuliza kulitesa kwa vipi? Hivi majangili wamo bungeni?

Jibu la swali la maoni haya laweza kuwa jepesi au gumu kwa kuwa yawezekana likajibiwa ‘ndiyo’ au likajibiwa ‘hapana’ pasipo kutaka kuzingatia takwimu za waliosema ndiyo au hapana. Lipo tatizo.

La muhimu kuzingatia hapa ni kuwa, hakika hatuna budi kuwa makini sana kwani Watanzania walio wengi kwa sasa si wale wa miaka ya 47, wanao upeo wa juu wa uelewa na wenye ufahamu wa kutosha kabisa, hivyo watambuzi na wadadisi wa kufahamu na kutambua mambo yao muhimu ya kitaifa na hali mbalimbali zenye mushkeli na zinazopelekwa kimzaha na kwa mazoea.

Ni mtazamo wangu kuwa huenda katika suala la ujangili ambalo ni moja ya tuhuma za makosa ya jinai linapobainika na kutolewa taarifa hususan hata kuwepo watuhumiwa waliokamatwa haipendezi kuona na kusikia utetezi mkubwa na mzito namna ile bungeni huku hata wabunge wenyewe wakianza kutuhumiana hadharani kuwafahamu wahusika.

Ni bora tukapingana na tukaparaganyika ovyo katika masuala ya itikadi za vyama kwa ngazi yake husika, lakini inapofika kwenye ngazi ya masuala ya masilahi ya kitaifa hatuna budi kuachana na tofauti zetu za itikadi za vyama na kuwa kitu kimoja (Bunge moja) kwa masilahi ya taifa.

Hakika ujangili ni janga kwa utalii wetu na ukichezewa chezewa kimzaha na kimazoea hivi hivi hakuna mnyama atakayesalimika nchini kwani mifano ipo mingi.


Maoni: 0758 999 777.



No comments:

Post a Comment