Thursday, November 28, 2013

TPSF:Kagasheki kuwa jasiri kukabili majangili



Na Mwandishi wetu
28th November 2013


Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki (wa pili kushoto), akiwa kwenye mazungumzo na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Reginald Mengi (wa tatu kushoto), jijini Dar es Salaam jana.
Taasisi ya Sekta Binafasi Tanzania (TPSF) imemshauri Waziri wa Mailiasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kuwa na moyo wa ujasiri kukabiliana na unjangili hasa wa kuua tembo kwa kuwa biashara ya pembe zake inafanywa na watu wakubwa.

Ushauri huo ulitolewa jana katika mkutano wa mashauriano kati ya sekta binafsi na Waziri Kagasheki ambayo mambo kadhaa ya ushirikiano baina ya serikali sekta hiyo yalijadiliwa.

TPSF pia iliitaka serikali kulinda hifadhi za misitu kwani miti imekuwa ikikatwa ovyo na kutoa mifano kwenye hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na Mufindi, mkoani Iringa.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na TPSF na kumwalika Waziri Kagasheki ukiwa ni mkakati wa kukuza ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali na kupeana ushauri juu ya namna ya kuzitumia rasilimali za taifa kwa ajili ya manufaa ya Watanzania, Balozi Kagasheki alisema kuwa sekta binafsi ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi na zisiposhirikishwa kikamlifu, serikali haiwezi kufika popote.

Ujumbe wa TPSF uliongozwa na Mwenyekiti wake, Dk. Reginald Mengi.

Balozi Kagasheki alitaka serikali isionekane kuwa ndiyo yenye kufanya mambo yote ikiwa ni pamoja na masuala yote ya kufanya maamuzi kwani inahitaji kuzishirikisha sekta binafsi na kwa kutofanya hivyo, hawawezi kufika popote.

Alisema serikali haiwezi kufanya biashara isipokuwa inaandaa mazingira kwani katika nchi yoyote, kwa sehemu kubwa wenye kuendesha  shughuli hizo ni sekta binafsi, hivyo mchango wao unahitajika kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini.

 “Nilipata barua pale ofisini, sekta binafsi ni chombo muhimu, hivyo nikaona kuna umuhimu wa kuja kwenye mkutano huu. Bado naamini kwamba kukiwa na uhusiano mzuri kati ya serikali na sekta binafsi, tutafika mbali,” alisema Kagasheki na kuongeza:

 “Ile ‘bureaucracy’ (urasimu) ya kuona wengine hawawezi kutunga sera wala kufanya maamuzi  ila ni serikali pekee, hatuwezi kusonga mbele wala kupiga hatua.
Ni lazima pawepo na ‘interaction’ (majadiliano ya pamoja), ‘participation’ (ushirikishwaji) kati ya serikali na sekta binafsi ili kuweza ‘ku-solve’ (kutatua) baadhi ya matatizo yanayojitokeza.” 

Waziri Kagasheki aliongeza kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti mapema kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinapojitokeza, kinyume cha hapo itapokea malalamiko.

Pia alitaka mazingira ya uwekezaji yaboreshwa ili kuwavutia wawekezaji kwani kinyume cha hilo, wanaweza kukatishwa tamaa.

Kwa upande wake, Dk. Mengi alimpongeza Balozi Kagasheki kwa kuonyesha kuijali sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kukubali kushiriki mazungumzo hayo ya kupeana ushauri juu ya kuzitumia vyema rasilimali zilizopo ikiwa ni  pamoja na uwekezaji wenye tija kwa taifa.

 “Kwa nini sekta za umma na za binafsi zinapokutana zinaonekana kama hazijatoka nchi moja?” alihoji na kuongeza: “Zinakuwa kama maadui.
Kuna fikra potofu ya kuona kwamba sekta binafsi ni wanyonyaji, lakini wewe (Waziri Kagasheki) unaonyesha  kuwa tupo pamoja.”

Dk. Mengi aliongeza kuwa: “Sekta binafsi zinaweza kusaidia kutia msukumo sekta ya maliasili ambayo kama yenyewe isingeweza… Tunakushukuru kwa kuanzisha hiyo ‘interactions’ (majadiliano ya pamoja) kwani sasa tunajiona tupo pamoja katika kujenga taifa letu.”

Aliitaka serikali kuwahamasisha Watanzania  juu ya umuhimu wa misitu kuwa ni biashara kwani mchango wa sekta ya misitu kwenye pato la taifa unakuwa mdogo kwa sababu wananchi hawajaelimishwa vya kutosha namna ya kuzitumia na kufaidika na rasilimali hizo.

Dk. Mengi vilevile aliitaka serikali kuweka mazingira mazuri ya sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo mazuri wanaofanya kazi kwenye eneo hilo huku ikipunguza gharama za utalii ili kupata watalii wengi wa ndani na nje.

Naye Juma Mgoo, kutoka sekta ya misitu wizarani hapo, alisema kuwa sera ya taifa ya sekta hiyo ya mwaka 1998, inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuendeleza rasilimali hizo nchini.

No comments:

Post a Comment