Sunday, November 24, 2013

JANGILI AJERUHI ASKARI WA TANAPA,


Novemba 24,2013.
Serengeti:ASKARI wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti Yusuph Namwandila amenusurika kufa na  amelezwa hospitali ya wilaya ya Nyerere baada ya kushambuliwa na jangili kwa simu na kumkata kichwani na  sikio,wakati wa kuwakamata.
Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Serengeti William Mwakilema ambaye yuko nje ya hifadhi kikazi ,uongozi wa hospitali ya wilaya wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo novemba 22 majira ya kati ya saa 4 na 5 usiku ndani ya hifadhi hiyo eneo la Bisarara kata ya Sedeco.
Akisimulia mkasa huo mkuu wa kituo cha Tabora B,mhifadhi Martini Magoko alisema jangili huyo akiwa na wenzake zaidi ya watano walikutwa ndani ya hifadhi na walipoamriwa kukaa chini ya ulinzi ,ghafla akachomoa sime na kumkata askari sehemu ya kisogo na sikio la kulia.
“Kutokana na kukithiri kwa ujangili usiku ,askari wanaweka doria …majangili walikuwa wengi na wanatembea kwa kuwasha tochi na kuzima…askari wangu wakaamua kubana sehemu ya kichuguu ambako walikuwa wanaelekea,…kukaribia kama hatua nane wakawekwa chini ya ulinzi…wakatawanyika na kukimbia…huyo mmoja akachomoa sime na kwa kuwa ilikuwa giza akamkata askari vibaya….alitarajia kumuua”alisema.
Alisema baada ya kushambuliwa alipiga kelele kuomba msaada na wenzake wakaaacha kuwafukuza wengine na kurudi kutoa msaada na kumkuta ana hali mbaya kwa kuwa damu ilivuja sana .
“Alikatwa mshipa na damu zikavuja sana….akaonekana kuzidiwa sana na kulazimika kumweka ndani ya gari na kumkimbiza hospitalini na kuongezewa damu”alisema Magoko.
Kuhusu kasi ya ujangili wa wanyama mbalimbali alisema unaendelea hasa wakati wa usiku kwa vijiji vilivyoko kando kando ya hifadhi hiyo,kutokana na kuhama kwa makundi makubwa ya nyumbu kutoka Kaskazini kwenda magharibi na Kusini .
“Majangili wanaingia na tochi za mwanga mkali na mapanga kipindi hiki… wanawamulika wanyama na kuwafukuza na kuwakata …wanaua wanyama wengi sana…na wengine wanaachwa humo hali ambayo ni hatari zaidi kwa uhifadhi”alisema.
Mhifadhi huyo ambaye ni mkuu wa kanda ya Kaskazini alibainisha kuwa kwa kipindi cha julai hadi sasa ambacho nyumbu huingia maeneo ya jilani na vijiji wamekamata majangili zaidi ya 200 wakiwemo watoto wadogo wa miaka 12-14 wanaotumiwa na wazazi katika maeneo hayo hasa kijiji cha Merenga kata ya Nyansurura.
Kwa upande wake Meneja uhusiano wa Tanapa Paskael Shelutete alisema kuwa mapambano ya ujangili ni makubwa na askari wako hatarini kupoteza maisha kutokana na hali ilivyo kwa kuwa wanafanya kazi usiku na mchana na katika mazingira magumu ,jamii na wadau wengine wanatakiwa kutambua na kuunga mkono juhudi za uhifadhi.
Mganga wa zamu hospitali ya Nyerere Nyanzirali Kitara alisema majeruhi anaendelea vizuri ,”kwa sasa hali zi mbaya,aliumizwa njia ya sikio na damu zikavuja nyingi…tumepiga picha hajaumia fuvu kwa hiyo hali yake si mbaya sana”alisema.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment