Friday, November 1, 2013

Majangili kutafutwa kwa teknolojia ya kisasa

  
na Dixon Busagaga, Moshi-Tanzania daima.

WATAALAMU wa usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori kutoka nchi zaidi ya 20 duniani wamekutana mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro kujadili matumizi ya teknolojia mpya ya kubaini majangili.

Hatua hiyo inakuja wakati huu ambao baadhi ya wabunge wamekuwa wakiituhumu serikali kuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua dhidi ya viongozi wake wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu.

Teknolojia hiyo ya kisayansi iliyoibuliwa nchini Marekani ijulikanayo kama Forensic Science Laboratory imekuja wakati sakata la ujangili likiwagawa wabunge na baadhi ya mawaziri wanaodaiwa kujihusisha na biashara hiyo.

Licha ya kuingizwa katika mitaala ya vyuo vya usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori nchini, itatumiwa na vikosi vya operesheni za ujangili vinavyojumuisha maofisa wa Usalama wa Taifa, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), askari wa wanyamapori, polisi na wataalamu wa vyuo vya wanyamapori.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 50 ya usimamizi, uhifadhi wa wanyamapori na utalii yanayoendelea katika Chuo cha Mweka, Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori nchini Kenya, Prof. George Otiang’a, alisema teknolojia hiyo imefanikiwa kutokomeza ujangili kwa kiasi kikubwa nchini Marekani na kwamba katika Bara la Afrika nchi ya Afrika Kusini ndiyo nchi pekee iliyoanza kuitumia.

Alisema kwa sasa wameanza mashauriano kuhusu teknolojia ya kisayansi ambayo inawawezesha askari na wataalamu wa masuala hayo kuwagundua majangili kupitia taarifa za vinasaba (DNA) kwa kupima damu ya mnyama.

Pia watapima alama za nyayo za majangili pamoja na alama za vidole vya majangili katika mwili wa mnyama aliyeuawa.

“Mbinu hiyo itaondoa utata wa kuwabaini wahusika kupitia taarifa za DNA, Kenya na Tanzania ndiyo tupo kwenye mchakato wa kuingiza aina hiyo ya utambuzi wa kisayansi kwenye mitaala ya vyuo vya usimamizi na uhifadhi wa wanyamapori ili kukabiliana na wimbi hili la ujangili wa tembo na faru Afrika ya Mashariki,” alisema.

Kwa mujibu wa Otiang’a, hali ni mbaya na kila nchi imekuwa ikijadili na Tanzania inaangalia uwezekano wa kuzishauri serikali za mataifa husika, ingawa teknolojia hiyo ni gharama kubwa kuiendesha.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na hatua hiyo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Usimamizi na Uhifadhi wa Wanyamapori Afrika (Mweka), Dk. Freddy Manonge, alisema hivi sasa Tanzania iko kwenye mchakato wa kuandaa mtaala unaotumia teknolojia ya kutambua wahalifu wa ujangili katika hifadhi zote zilizopo hapa nchini ili kuondoa kigugumizi cha kukwepa kuwashughulikia wahusika wa ujangili ambao wameiweka rehani rasilimali hiyo adimu.

Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Dk. Alex Kissingo, alisema tatizo la ujangili wa wanyapori nchini ni kubwa na kwamba wengi ambao wamekuwa wakikamatwa kwa matukio hayo ni watumishi wa serikali na hifadhi za wanyamapori.

Naye Dk. David Manyanza ambaye aliwahi kuwa mkuu wa chuo hicho, alisema vita dhidi ya ujangili inaonekana kuwa ngumu kutokana na usiri unaotumika katika biashara hiyo pamoja na kuwapo kwa mkono wa watu mashuhuri wakiwamo viongozi wa juu ndani ya serikali.

Alisema ikiwa kutakuwa na utashi wa dhati katika mapambano haya kutoka kwa wananchi wenyewe, serikali pamoja na wafanyabiashara, tatizo la ujangili linaweza kumalizika.


No comments:

Post a Comment