Saturday, November 2, 2013

Kijiji kilichoonja chungu ya kutokomeza ujangili



Charles Ndagulla-Tanzania daima

OKTOBA 13, mwaka huu ni siku iliyovuruga mwenendo wa maisha ya kila siku ya wananchi wa Kijiji cha Minziro kilichopo Kata ya Minziro, Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera baada ya kundi la wanajeshi wanaoendesha Operesheni Tokomeza Ujangili kuvamia kijiji hicho.
Kabla ya mkasa huo, siku hiyo ilikuwa tulivu. Waumini wa madhehebu mbalimbali waliamka asubuhi na mapema kwenda kumwabudu muumba wao kama ilivyo ada kila Jumapili.
Wakati waumini hawa wakirejea majumbani baada ya kutoka kwenye ibada, walikutana na upepo mbaya, na huu si ule unaoezua mapaa ya nyumba wala kung’oa miti, bali ni wa kipigo kutoka kwa walinda amani wetu.
Kila mmoja alikimbia kivyake kuokoa nafsi yake, na wale walioshindwa kuhimili mikiki ya mbio waliangukia mikononi mwa wapiganaji wetu, na hapo ndipo vipigo vilianza bila kuangalia sehemu ya kupiga.
Makamanda hawa hawakuishia kutembeza vichapo kwa raia wema tu, bali walienda mbali kwa kuchoma moto  baadhi ya nyumba za wananchi hao. Hakika Minziro iligeuka uwanja wa vita.
Wananchi hawa hadi sasa wamejawa na hofu, hawamwamini mtu yeyote wasiyemfahamu, na kila wamuonapo wanajificha kwenye mashamba ya migomba na baadhi yao vichakani wakitafakari kitakachotokea tena kwa siku hiyo.
Ni wachache waliothubutu kuwasogelea wanahabari waliotinga kijijini hapo kupata taarifa sahihi juu ya mkasa huo, lakini bado walikuwa wamejawa na hofu hadi hapo walipotolewa hofu hiyo na wenyeji walioambatana na wageni hao.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mulungu A, Boniface Ponsian, ambaye ni mmoja wa wahanga wa tukio hilo baada ya kukamatwa na kushitakiwa kwa madai ya kumiliki mazao ya misitu bila kibali, anasema hali bado ni tete kijijini hapo.
Anasema hadi sasa wananchi wengi wameyahama makazi yao na kukimbilia mafichoni, huku wakiwaacha watoto wadogo wakiwa hawana msaada wa wazazi wao.
Katika tukio hilo, wanajeshi hao wanadaiwa kuwafunga kamba wananchi na kuwaning’iniza kwenye magari yao wakiwa wamewainamisha vichwa chini, huku baadhi yao wanadaiwa kutapika kutokana na mtikisiko wa magari.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, zaidi ya wananchi 20 wa Kijiji cha Minziro waliumizwa vibaya na askari hao wanaodaiwa kuwapa mateso ya kila aina wakiwahusisha na wahamiaji haramu kutoka nchi za Burundi, Rwanda na Uganda na uvunaji wa mazao ya misitu kutoka msitu wa hifadhi ya taifa wa Minziro.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa kitongoji, wanajeshi hao baada ya kutembeza kipigo kwa wananchi kwa siku mbili mfululizo, walichoma moto nyumba yakiwamo maduka na kubomoa baadhi ya milango ya nyumba hizo.
Mwenyekiti huyo amewataja baadhi ya wahanga walioshambuliwa na askari hao kuwa ni Josephat Joseph, Edwin George, Didas Domisheni, Steven Serapioni, Sonko Yoronimu, Mkasa Mathias na Josephat Emmanuel.
Wanajeshi hao walichoma moto duka la mfanyabiashara Joseph Jovin wa Kijiji cha Minziro ambaye amekimbia makazi yake sanjari na Edward Mgowa ambaye alibomolewa milango ya nyumba yake na mwenyewe amekimbilia kusikojulikana yeye na mkewe na kuacha watoto wao watano wakiwa wapweke.
Katika tukio hilo, askari hao walimuumiza Josephat Emmanuel baada ya kupewa adhabu ya kutembelea magoti kwa umbali mrefu.
Pamoja na ukweli kwamba vyombo vya ulinzi na usalama Wilaya ya Misenyi vinafahamu operesheni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali mstaafu Issa Njiku, anadai hana taarifa yoyote juu ya tukio hilo.
Kwa mtu wa kawaida, anaweza akahisi  mkuu hyo wa wilaya haelewi wajibu wake, lakini ukweli ni kwamba anaficha uoza uliofanywa na walinzi hao wa amani ama kwa makusudi ama kwa kutokufahamu.
Si mkuu wa wilaya pekee, hata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Phillp Kalangi naye usemi wake ni huo huo wa DC Njiku, kwamba hana taarifa kutoka kwa OCD wake wa Misenyi, Yusuf Mtatifikolo, juu ya tukio hilo ikiwa ni wiki tatu zimepita tangu litokee.
Tukio hilo halikuishia siku moja, liliendelea siku ya pili ya Oktoba 14, ambako viongozi wa serikali ya kijiji hicho walikamatwa na kuwekwa mahabusu polisi kwa siku tano kabla ya kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa ndani ya siku mbili.
Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Minziro, John Sali Kilibwa, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mulungu A, Ponsian na Anastazia Nestory ambao walihukumiwa Oktoba 22, mwaka huu kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya sh milioni moja kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki mazao ya misitu bila kibali. Walilipa faini.
Wakati viongozi hao wakinusurika kwenda gerezani kutumikia kifungo, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Minziro, yeye alikwenda gerezani baada ya kujikuta akikamatwa muda mfupi tu baada ya kuwatolea ushahidi viongozi hao wa kijiji. Amefunguliwa mashitaka matatu; kuvuna mazao ya misitu bila kibali, kusafrisha mazao ya misitu bila kibali na kumiliki mazao ya misitu kinyuume cha sheria. Kesi yake bado inaendelea.
Kwa muundo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa, Kanali mstaafu Massawe, ndiye mwenyekiti wake na katibu ni Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Mkoa (RSO). Ndivyo hivyo na wilayani ambako DC Njiku ni mwenyekiti wa kamati na katibu wake ni DSO.
Mbali na wanajeshi, wengine waliokuwa wakitekeleza operesheni ya kuwashambulia wananchi wa Kijiji cha Minziro na vitongoji vyake wanatoka  kwenye Idara ya Usalama wa Taifa, polisi na maofisa kutoka Idara ya Misitu ambayo kwa sasa inaitwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.
Swali ni je, nani atawaondolea hofu na mashaka wananchi hao wa Kijiji cha Minziro na vitongji vyake pamoja na vijiji jirani? Kwani hadi naandika makala hii, wanajeshi hao wangali wakivinjari kijijini hapo wakiwasaka watu waliowaumiza wenyewe kwa sababu wanazozifahamu wenyewe.
ndagullacharles@yahoo.com 078

No comments:

Post a Comment