na Jumbe Ismailly, Singida-Tanzania daima
|
WATU wawili, akiwemo askari polisi, wameuawa
katika Kitongoji cha Kirumbi, Kijiji cha Kintanula, Kata ya Mwamagembe,
mkoani Singida wakati wakirushiana risasi na kundi la majangili wanaodaiwa
kujihusisha na vitendo vya biashara haramu ya nyara za serikali.
Tukio hilo lilitokea wakati askari huyo akirejea
nyumbani wilayani Manyoni, usiku wa kuamkia Oktoba 31, akitokea katika
Operesheni Tokomeza Ujangili inayoendelea wilayani Manyoni, mwaka huu.
Askari aliyeuawa ni mwenye namba G.9934 D/C Mgaka
(26) huku mtuhumiwa wa ujangili akitambulika kwa jina la Selemani Kimpinde
maarufu kwa jina la “Masta”, mkazi wa Kijiji cha Kipili, Kata ya Sikonge
mkoani Tabora.
Inadaiwa kuwa baada ya askari wa kikosi maalumu
cha Operesheni Tokomeza Ujangili kumkamata mtuhumiwa na pikipiki aliyokuwa
akitumia katika matukio ya ujangili, aliwaomba kwenda kuwaonyesha mahali
zilipo silaha wanazotumia kufanyia vitendo hivyo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Fatma Taofiq, alithibitisha
tukio hilo akisema baada ya askari huyo kumkamata mtuhumiwa walipanda gari na
kuanza safari ya kwenda kuonyeshwa zilipo silaha aina ya SMG, lakini
walipofika mita kama 100 kabla ya kufika kwenye eneo husika, askari hao
waliamua kushuka kwenye gari na kuanza kutembea kwa miguu.
Alisema kuwa baada ya kufika kwenye eneo ambalo
walitegemea kuonyeshwa silaha, alitokea jangili mmoja aliyekwenda kumpora
askari silaha aliyokuwanayo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo, wakati wa purukushani na
jangili hilo lililomnyang’anya silaha askari, walijitokeza majangili
wengine wawili na kumpiga risasi askari huyo.
Alisema baada ya askari huyo kuanguka chini
akiugulia maumivu, ndipo jangili huyo alianza kutimua mbio mara tu baada ya
tukio hilo.
Kwamba wakati likitimua mbio, askari wengine
waliokuwa wamejificha, mmoja wao alimpiga risasi na kufa papo hapo.
Mkuu huyo wa wilaya aliwapongeza askari
wanaofanya kazi hiyo kwa kile alichodai kuwa operesheni hiyo imefanikiwa kwa
kiasi kikubwa sana na bado wanaendelea kuwasaka majangili waliokimbia mara
baada ya kutenda tukio hilo.
|
Saturday, November 2, 2013
Jangili aua askari Singida
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment