Wednesday, October 30, 2013

Ujangili walitesa Bunge

chanzo Tanzania daima 

TUHUMA za ujangili na Operesheni Tokomeza UIjangili inayoendeshwa na serikali, jana ziliiteka Bunge baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kuituhumu serikali kwa kutoa hoja nyepesi bungeni.
Lugola alisema operesheni hiyo inafanyika kwa kukiuka haki za binadamu, kwamba watu wasiokuwa majangili wamekamatwa, kuteswa na kuharibiwa mali zao ilhali majangili wanaojulikana wakiachwa waendelee na uhalifu wao.
Wakati mbunge huyo akitoa tuhuma hizo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliwatuhumu wabunge na wanasiasa wengine kwa kuingilia utendaji wa operesheni hiyo kwa kuwatetea wanaokamatwa kwa kujihusisha na ujangili.
Kauli ya Nahodha ilionekana kumpiga kijembe Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye wiki iliyopita msaidizi wake (ofisi ya ubunge) alikamatwa mkoani Iringa kwa tuhuma za ujangili.
Jana Lukuvi alidai anao ushahidi ‘mzito’ wa mateso aliyoyapata msaidizi wa ofisi yake, ambaye aliachiwa juzi baada ya kuonekana kutohusika na ujangili kama ilivyokuwa ikidhaniwa.
Hoja ilivyoanza
Hoja hiyo ilitokana na swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), aliyetaka kujua kwanini serikali inaendelea kuwalinda wanasiasa, askari na watendaji wake wanaojihusisha na ujangili.
Lembeli pia alitaka kujua kwanini serikali haiwachukulii hatua za kisheria makamanda wa polisi wa mipakani, hasa wale wanaopakana na mbuga ya Serengeti, wanaojihusisha na ujangili, kutorosha nyara za serikali pamoja na kushirikiana na majangili.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Mazingira, Lazaro Nyalandu, alisema kamwe wizara yake haiwalindi wanasiasa, wabunge, maofisa wa polisi na watendaji wa serikali wanaohusika na ujangili.
Nyalandu alisema kuanzia sasa kila kiongozi atakayekamatwa kwa tuhuma za ujangili atatangazwa hadharani.
Alisema si sahihi kuwatuhumu wabunge, polisi na watendaji wengine wa serikali bila ya kuwa na utafiti juu ya tuhuma zao.
Hoja ya Lugola
Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Lugola aliomba mwongozo wa spika akitumia kanuni ya Bunge ya 67, ambapo alilitaka Bunge liiagize serikali kutoa taarifa ya operesheni hiyo inayofanyika nchi nzima.
Lugola aliomba mwongozo huo akisema kuwa majibu ya Waziri Nahodha na Nyalandu juu ya suala hilo ni ya mzaha mzaha yenye lengo la kuendeleza kulindana.
Mbunge huyo alilitaka Bunge liilazimishe serikali kutoa taarifa rasmi juu ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Mara baada ya Lugola, kuzungumza alisimama Lukuvi ambaye alitaka serikali iachwe imalize operesheni hiyo bila kutoa taarifa kwani wakifanya hivyo wanaweza kusababisha wahusika wakimbie au kupoteza ushahidi.
Alisema  taarifa za operesheni hiyo zitapelekwa katika kamati zinazohusika mara baada ya kufikia tamati na baadae zitafikishwa bungeni kulingana na taratibu zinazotakiwa.
Lukuvi pia alionyesha simu yake ya mkononi akidai ina ushahidi wa mateso yanayofanywa dhidi ya wanaokamatwa kwa tuhuma za ujangili.
“Nina ushahidi wa msaidizi wangu alivyoteswa baada ya kukamatwa kuwa ni jangili, huyu wamemuachia jana, nawaombeni tuache operesheni hii imalizike ndipo tupatiwe taarifa zake,” alisema.
Naibu Spika Job Ndugai, aliunga mkono kauli ya Lukuvi akidai taarifa za operesheni hiyo zikitolewa sasa zitaharibu zoezi hilo.
Hoja ya Lema
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amesema anatarajia kuwasilisha maelezo binafsi bungeni kuitaka serikali izuie uwindaji wa tembo katika vitalu vilivyo karibu na hifadhi au mbuga.
Lema alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na ujangili kuzidi kushika kasi. Inakadiriwa tembo 30 wanauawa kila siku.



No comments:

Post a Comment