Kagasheki
amfikisha RCO kwa IGP
na
Grace Macha, Arusha
|
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema kuwa suala la Mkuu
wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha (RCO), Duwan Nyanda, anayetuhumiwa kutorosha
watuhumiwa wa ujangili linashughulikiwa na Inspekta Jenerali wa Jeshi la
Polisi (IGP), Saidi Mwema.
Mwishoni
mwa wiki iliyopita, Kagasheki alimtuhumu RCO huyo kuhujumu operesheni
‘Tokomeza Majangili’, baada ya kudaiwa kuwatorosha majangili wawili raia wa
kigeni.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Arusha, Kagasheki alisema kuwa vita dhidi
ya ujangili wa meno ya tembo inayotishia kutoweka kwa wanyama hao haitakoma
mpaka majangili hao waache.
Aliongeza
kuwa watumishi wa serikali wanaowasaidia majangili hao wanasukumwa na
ubinafsi kwa kuamua kujinufaisha binafsi na rasilimali hizo za umma.
Alisema
operesheni hiyo ya ‘Tokomeza Ujangili’ iliyoanza hivi karibuni inahusisha
majeshi yote ya ulinzi na usalama.
RCO
Nyanda anadaiwa kusaidia kuwatorosha watu wawili wenye uraia wa Saudi Arabia
ambao walikuwa wakishikiliwa baada ya kukutwa wakiwa na silaha na baadhi ya
vithibitisho vinavyoonesha walikuwa majangili.
“Inasikitisha
sana na inaturudisha nyuma ikiwa kama kiongozi wa jeshi anayevaa sare ya Watanzania,
kwa makusudi anawaachia watuhumiwa wa ujangili na kusaidia kuondoka nchini,”
alisema Kagasheki wakati akizungumza na waandishi mwishoni mwa wiki.
Alisema
katika tukio hilo, polisi walifanikiwa kuwakamata watu hao wakiwa na
vithibitisho vyote vya kujihusisha na ujangili na kuwapeleka kituo cha polisi
Arusha kwa ajili ya mahojiano.
Alifafanua
kuwa kabla ya kuwekwa rumande, watu hao walinyang’anywa hati zao za kusafiria
ili kuwazuia wasitoroke. Lakini katika hali ya kushangaza RCO Nyanda
alihakikisha anawatoa nje kwa dhamana na kisha aliwakabidhi hati hizo kitu
kilichosababisha watoroke nchini.
Mapema
akifungua mkutano wa mwaka wa Chama cha Mashirika ya Utangazaji ya Kusini mwa
Afrika (Saba) jijini hapa jana, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal,
alivitaka vyombo vya habari vya nchi hizo kujikita katika kutangaza vivutio
vilivyopo.
Alisema
lengo ni kuongeza idadi ya watalii watakaovutiwa kuvitembelea ili kukuza
uchumi wa nchi zao.
Pia
vimetakiwa kuandaa vipindi vya maendeleo ikiwamo kutangaza vivutio vya
kiutamaduni ambapo mbali na kuyaingizia mapato mataifa yao kutawezesha
kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa maeneo husika.
Alisema
kuwa vyombo vya habari ni muhimu katika kuelimisha na kuburudisha lakini
vikitumiwa vizuri vinaweza kuchangia kuleta maendeleo ikiwamo sekta ya
utalii.
Dk.
Bilal alisema suala la kutangaza vivutio vya Afrika lisiachiwe vyombo vya
habari vya nje ya bara pekee ambavyo huwashawishi watalii kwenda maeneo
wanayoyataka wao, bali vitangaze maeneo yote kwa kueleza uzuri wake.
Alivitaka
vyombo hivyo kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa uhifadhi na ulinzi wa
vivutio vya maliasili badala ya kusubiri ziharibike ndipo vianze kutoa
taarifa za madhara.
Dk.
Bilal alivitaka vyombo vya habari nchini kuungana na serikali katika kukabiliana
na ujangili ili kuhakikisha unamalizika kabisa.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), Allan Kijazi, alisema
tayari wamekamilisha taratibu za Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa
Mawasiliano nchini (TCRA) ili waruhusiwe kuandaa filamu za wanyamapori.
Alisema
kuwa kwa sasa ni watu kutoka mataifa ya Ulaya ndio hufika kwa ajili ya
kuandaa filamu hizo, hivyo kukamilika kwa taratibu ni fursa kwa shirika hilo
kuanza kuandaa filamu hizo zikionesha na kuzungumzia vivutio vyote vya utalii
vilivyoko nchini.
Kijazi
alisema kwa sasa ni vivutio vichache tu ndivyo vinavyotambuliwa huku vingi
vikiwa vimeachwa, jambo alilotaka kuwepo na mwamko miongoni mwa wanahabari
kuvitangaza kwa kufuatilia ni kitu gani kipya kinaendelea kwenye sekta ya
utalii na kuvitangaza kwa usahihi.
Mkutano
huo wa siku nne unahudhuriwa na washiriki kutoka nchi 14 za SADCC, ambapo pia
ulihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Prof. Makame
Mbarawa.
|
Tuesday, October 22, 2013
RCO ALIYETOROSHA WATUHUMIWA WA UJANGILI ASHITAKIWA KWA IGP
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment