Na Mwandishi wetu
|
RAIS Jakaya Kikwete ametangaza kuwa ataliamrisha
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuongoza mapambano dhidi ya ujangili wa
tembo na faru na ukataji haramu wa miti kwa shughuli za biashara ambao
umefikia kiwango kikubwa nchini.
Alisema kuwa sekta ya utalii nchini sasa imeanza
kutishiwa na uvunaji wa wanyama hao na biashara haramu ya meno ya tembo na
faru, na kwamba tishio hilo ni kubwa kwa sababu sekta hiyo inachangia kiasi
cha asilimia 17 katika mapato ya taifa na inaajiri watu 300,000.
Rais Kikwete alitangaza uamuzi huo juzi wakati
alipozungumza kwenye mkutano wa viongozi wa nchi na serikali kuhusu biashara
haramu ya wanyama na bidhaa zake pamoja na biashara haramu ya bidhaa za miti
na mbao jijini New York, Marekani.
Aliuambia mkutano huo, ulioandaliwa na Rais Ali
Omar Bongo Ondimba wa Gabon na Serikali ya Ujerumani kwenye Makao Makao ya
Umoja wa Mataifa kuwa mwaka 1960, Tanzania ilikuwa na tembo 350,000 lakini
kutokana na ujangili idadi hiyo ilishuka hadi 110,000 ilipofika mwaka 2009.
Kuhusu faru, Rais Kikwete alisema kuwa mwaka 1974
walikuwepo 700 na sasa wako chini ya 100 kwa sababu ya vitendo vya kijangili.
“Katika miaka ya 1980 na 1990 wakati wa kilele
cha ujangili katika mikonga ya wanyama, tulilazimika kutumia jeshi kutuliza
hali hiyo. Tuliona matokeo mazuri na tulikuwa na utulivu wa aina fulani.
“Lakini katika miaka minne iliyopita,
tumeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ujangili kwa ari na kasi mpya. Kwa
mfano kati ya mwaka 2010 na Julai, 2013, zaidi ya tembo 1,386 waliuawa
nchini,” alisema.
Rais Kikwete aliongeza kuwa wamechukua hatua kali
za kupambana na ujangili ikiwa ni pamoja na kurekebisha sera, sheria na
kanuni.
Aliongeza kuwa wamesaini mikataba mbalimbali ya
kimataifa ya kupambana na ujangili huu.
“Vile vile, tumechukua hatua za kukamata
majangili na hata kukamata silaha zinazotumika katika ujangili. Kati ya mwaka
2010 hadi katikati ya mwaka huu, majangili 5,189 wametiwa mbaroni na silaha
1,952 zimekamatwa.
“Isitoshe vipande 3,788 vya meno ya tembo vyenye
uzito wa kilo 10,756 vilikamatwa nchini. Nimeamuru JWTZ kukabiliana na hali
hiyo na naamini kuwa tutapata mafanikio makubwa zaidi katika operesheni
inayoandaliwa,” alisema.
Wakati huo huo, Rais Kikwete alisema kuwa mifuko
ya hifadhi nchini itaendelea kuchangia maendeleo kwa kugharamia miradi
mbalimbali, lakini kwa namna ya kuilinda ili serikali isije kuua ‘bata wa
dhahabu anayetaga mayai ya dhahabu’.
Rais alisema kuwa misaada inayotolewa na Shirika
la Misaada ya Maendeleo la Marekani (MCC) ni ya aina yake duniani kwa sababu
wanufaika wakubwa wanapewa uhuru wa kuamua ni miradi gani ndani ya nchi
igharamiwe na misaada hiyo.
Vile vile, Rais Kikwete alizitaja sekta kubwa
ambako wawekezaji kutoka Marekani wanaweza kuwekeza mitaji yao kama njia ya
kuongeza uwekezaji wao katika Tanzania, na hivyo kusaidia kukuza kwa kasi
zaidi uchumi wake.
|
No comments:
Post a Comment