Makala
Toleo la 404
6 May 2015
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa nchini Tanzania
(Tanapa) limekanusha ripoti iliyotolewa na shirika la ITV nchini Uingereza
inayosema idadi ya tembo imekuwa ikipungua katika mbuga yetu ya Ruaha.ITV imetoa ripoti inayosema tembo wanauliwa kwa wingi nchini Tanzania, hasa katika mbuga ya Ruaha ambako idadi ya tembo imepungua kutoka 8,500 mwaka 2014 hadi 4,200 hivi sasa. Ripoti inasema sababu ya kupungua kwa tembo ni ujangili
Ripoti hiyo ni matokeo ya zoezi la miaka miwili la kuhesabu idadi ya tembo katika mbuga za Afrika kwa kutumia ndege maalumu.
Tanapa imesema haikuarifiwa kuhusu zoezi hili la kuhesabu tembo. Ikaongeza kuwa hata hivyo wanyamapori huwa wanahamahama kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Yaani kupugua kwao si lazima iwe kwa sababu ya ujangili
Wakati Tanapa inakanusha ripoti ya ITV, miaka miwili iliyopita Wizara ya Maliasili na Utalii ilitoa takwimu ikisema nusu ya tembo 20,000 wanaouawa katika Afrika nusu yake wanauliwa Tanzania. Kwa maneno mengine tembo 10,000 wanauawa na majangili kila mwaka. Matokeo yake idadi ya tembo imepungua kutoka 130,000 miaka kumi iliyopita hadi 70,000 mwaka 2013.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aliziomba nchi za Kiasia kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu ili kuzuia ujangili katika nchi yetu
Nadhani Nyalandu angepaswa pia kuuliza inakuwaje pembe hizi zinatoka nchini mwetu. Nani anawajibika au anawajibishwa? Suali hili si gumu kulijibu
Kwani mara nyingi tunapozungumzia ujangili na majangili tunasahau kuwa haiwezekani kwa biashara hii ya kimataifa kuendeshwa bila ya matajiri wakubwa, bila ya vigogo wa ujangili ambao wanafadhili na kugharamia wizi huu wa maliasili yetu
Jambo hili linaeleweka vizuri. Ndio maana serikali imesema mara kadha kuwa haitasita kuwataja hadharani vigogo wanaofadhili na kusafirisha pembe za ndovu kwa njia ya kificho. Waziri Nyalandu mwenyewe amesema hayo tangu alipokuwa Naibu Waziri.
Alisema mpango huo wa kuwaumbua watu wanaofadhili ujangili ama kusafirisha meno ya tembo, utakolezwa na mbinu mpya za kiintelijensia ambazo zitatumika katika ‘Operesheni Uhai’.
Suali la kujiuliza ni, je baada ya hiyo operesheni serikali imewaelewa vigogo hao? Je imeweza kuwakamata? Jibu analo Nyalandu.
“Wanaofadhili shughuli za ujangili tutawatangaza majina yao hadharani katika kukabiliana na tatizo hili. Lakini pia wageni wote watakaokamatwa nchini kutokana na ujangili tutawafukuza ndani ya saa 24 tena watapaswa kulipa nauli za ndege kwa gharama zao baada ya kutumikia adhabu watakazopata kwa mujibu wa sheria,” alisema Nyalandu.
Je Nyalandu aliwatangaza? Je, ni wageni wangapi wa aina hiyo wametumikia adhabu na kisha kufukuzwa nchi?
Nyalandu akaongeza kuwa wimbi la ujangili nchini limekuwa kubwa kutokana na majangili hao kusaidiwa na baadhi ya maofisa na wafanyakazi walioko kwenye vitengo vya ulinzi na usalama, kwa kuwa suala zima la usafirishaji wa pembe za ndovu hauwezi kuvuka kwenye mikoa husika pamoja na hifadhi zetu hadi kwenda bandarini wasikamatwe au kufahamika kama baadhi ya watendaji hawausiki.
Je ni maofisa wangapi wa aina hiyo wamefikishwa mahakamani na wangapi wamehukumiwa kifungo cha jela na mali zao kufilisiwa? Au Nyalandu anaishia kutoa ahadi tu?
Kuhusu suala la vigogo wa ujangili, haya yalisemwa tangu 2013 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Utalii, James Lembeli. Alisema kuna kila dalili kwamba baadhi ya vigogo serikalini wanahusika na biashara ya meno ya tembo nchini.
Akatoa mfano wa watu tisa waliokamatwa na meno ya tembo, wawili kati yao wakiwa polisi wa kituo cha Oysterbay, waliokamatwa Kisarawe, mkoani Pwani, wakisafirisha meno 70 ya tembo kinyume cha sheria. Huu ni mfano mdogo unaonyosha kidole kwa maofisa na vigogo
Akatoa mfano mwingine wa raia wa Uingereza, Robert Dewar aliyekamatwa nchini akiwa na nyara za serikali zenye thamani ya sh 118,314,900.
Mgeni huyo ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Trans Afrikas Longistics (TALL) alikamatwa na vipande vya meno ya tembo, meno ya tembo, meno ya simba, kucha za simba, ndege aina ya kasuku, vipande vya miti ya mpingo na idadi kubwa ya vinyago.
Mimi sina hakika kesi ya Dewar imefikia wapi, kama imemalizika au inaendelea. Kama imemalizika ni uamuzi upi uliotolewa na mahakama?
Kuhusu vigogo wa ujangili, wabunge nao waliwahi kuchachamaa na kushinikiza kutolewa kwa orodha ya vigogo hao. Walitaka kutajwa kwa majina ya mawaziri, viongozi wa serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara hiyo.
Mbunge mmoja alisema, “Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka. Mathalani, zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na mbuga ya Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao wakichukuliwa hatua”.
Nyalandu naye alisema Jeshi la Polisi ni vinara miongoni mwa makundi manne ya majeshi ambayo watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili.
Na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha akizungumza bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu, alikiri kuwapo fununu za wanasiasa ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo na kusema serikali italifanyia kazi jambo hilo.
Je imekwishalifanyia kazi au bado? Itachukua muda gani? Serikali imefikia wapi? Au Nahodha alikuwa akitoa majibu mepesi kama kawaida yao?
Tatizo hili pia lilizungumzwa na Rais Jakaya Kikwete alipohojiwa na mashirika ya kimataifa ya habari ya CNN na BBC. Alisema mtandao wa majangili unajulikana na jitihada za serikali zimefanikiwa kukamata vigogo 40 walio kwenye mtandao mkubwa wa biashara ya nyara za serikali.
Akaongeza kuwa watuhumiwa hao wamebainika kuwa wanajihusisha na mtandao na kwamba tajiri mkuu wa biashara hiyo naye amefahamika na kwamba anapatikana mkoani Arusha.
“Tumeutambua mtandao huo hadi wakubwa zao ni matajari pale Arusha kuna mmoja mkubwa ambaye sitaki kumtaja jina alikuwa akiendesha biashara hiyo naye yupo kwenye kundi hili la watu 40. Kazi iliyokuwa ikifanyika ni kuutambua huo mtandao kwa upana,” alisema.
Kuhusu athari za ujangili nchini, alisema baada ya Uhuru Tanzania ilikuwa na tembo wengi zaidi barani Afrika na hata duniani. Wakati huo walikuwa 350,000 na ilipofikia mwaka 1987 walipungua hadi 55,000.
Haya ni maneno mazito, hasa yanapotamkwa na mkuu wa nchi. Kitu gani kinafanya mkuu huyo ashindwe kuchukua hatua za kisheria na kuwaadhibu hao vigogo 40 waliotambulika? Kama kweli mtandao unajulikana na vigogo wanajulikana sasa iweje waendelee kutamba?
Kwani tunaambiwa kuwa baadhi ya mahakimu, polisi na waendesha mashtaka ni wahusika wakuu wa ujangili na biashara ya nyara za serikali. Tembo wapatao 30 huuawa kila mwezi na mtandao wa ujangili ambao unaundwa na wafanyabiashara wakuu ndani na nje ya nchi, wanaoshirikiana na baadhi ya maofisa na askari wa wanyamapori.
Ingawa Tanapa imekanusha ripoti ya ITV (Uingereza), Mkurugenzi Mtendaji wake, Allan Kijazi, amekiri kuwa hali ni mbaya, kuwa wahalifu wanapokamatwa wamekuwa wakiachiwa kinyemela “hata pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani”.
Wachunguzi wamebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa ambao wamewahi kunaswa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ujangili, wametoweka katika njia za kutatanisha na kuacha kesi zikiendelea.
“Ujangili huu ni mtandao mkubwa sana. Wanatumia silaha za kisasa zaidi kuliko hata za kwetu. Sisi hatupewi kibali cha kununua silaha hizo,” alisema Kijazi.
Ndipo inabidi tujiulize, hivi ile Operesheni Tokomeza kweli ilisaidia? Ikiwa Operesheni Uhai ilishindwa na hii ya Tokomeza nayo imelaaniwa kwa jinsi ilivyoendeshwa, ni vizuri tukajiangalia upya tulipokosea
Alipokuwa waziri wa nchi katika ofisi ya waziri mkuu, William Lukuvi alikiri mbele ya bunge kuwapo kwa vitendo vya utesaji wa watu waliokamatwa katika operesheni tokomeza.
Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa msaidizi wake jimboni ambaye alipigwa na kuteswa na askari kabla ya kuachiwa baada ya kushikiliwa kwa siku moja. Iwapo msaidizi wa waziri alitendewa unyama huo sembuse mwanakijiji wa kawaida
Alipoulizwa lini ripoti ya operesheni hiyo itawasilishwa bungeni, alisema, “Nadhani kuwa kuleta ripoti hivi sasa haitakuwa vizuri. Ni vizuri tusubiri mpaka kazi hii ikamilike na nina uhakika kuwa wizara itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwenye kamati husika.”
Tarahe 10 Aprili mwaka huu taarifa kutoka Ikulu ilituambia kuwa Rais Kikwete amepokea ripoti ya uchunguzi wa Operesheni Tokomeza kutoka tume ya uchunguzi aliyoiteua mwaka mmoja uliopita
Rais akasema serikali itaisoma ripoti hiyo na katika wiki mbili itatoa maelezo ya jinsi ripoti hiyo itakavyoshughulikiwa. Sina hakika kama baada ya wiki mbili maelezo hayo yalitolewa.
Hadidu za rejea ziliitaka tume hiyo ichunguze tuhuma mbali mbali za uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu za Operesheni Tokomeza.
Bila shaka wananchi wanasubiri kwa shauku kujua iwapo tume hiyoiliyoongozwa na Jaji (mstaafu) Hamisi Msumi imetimiza jukumu lake na iwapo serikali itatekeleza mapendekezo ya tume.
Tufuatilie mtandaoni:
Wasiliana na
mwandishi
+255-713562181
No comments:
Post a Comment