Friday, March 6, 2015

Kukauka mto Ruaha Mkuu pigo kiuchumi.




Na Abdallah Bawazir
6th March 2015
 
Tembo huyo wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni miongoni wa viumbe waliopo katika hatari ya kuangamia kutokana na athari za maji kukauka katika Mto Ruaja Mkuu.
Mto wa Ruaha Mkuu uliopo katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya hautiririshi maji tena, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma hasa majira ya  kiangazi.

Upungufu wa  maji katika mto huo, umesababisha athari kubwa kwa shughuli za kiuchumi zinazotegemea mto huo zikiwamo kilimo, uvuvi, uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na Kihansi na  maisha ya wanyama na sekta ya utalii kwa ujumla kutokana na kupita katika hifadhi ya Taifa Ruaha kubwa kabisa nchini.

Sehemu kubwa ya mto huo, iliyopo katika  mikoa ya Iringa (asilimia 40), Njombe (asilimia 15), Mbeya (asilimia 40) na Dodoma (asilimia 5), imekauka. Maji yakionekana yametuwama na kutengeneza madimbwi na katika baadhi ya maeneo yakitiririka kwa kasi ndogo, tofauti na hali yake ya kawaida yanapokuwapo ya kutosha.

Kwa ufupi, endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuunusuru, utakauka kabisa na kuwa pigo kubwa la kiuchumi si tu kwa wakazi wa maeneo hayo, bali taifa zima na sekta ya utalii ambayo inaelezwa kuongoza kuingiza fedha nyingi za kigeni katika pato la taifa. Hivi karibuni viongozi wa maeneo ambayo Mto Ruaha Mkuu unapita akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk. Rehema Nchimbi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro ambaye aliyewakilishwa, pamoja na wakuu wa wilaya za Kilolo, Ludewa, Iringa, Wanging’ombe, Makete na Njombe, walifanya ziara ya kutembelea maeneo ya mto huo, katika Hifadhi ya Ruaha na kushtushwa na hali ilivyo baada ya kujionea jinsi ulivyokauka na wanyama wanavyoathirika kwa kukosa maji.

Ziara hiyo iliandaliwa na Shirika la Uhifadhi Duniani (WWF) kwa kushirikiana na Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji, ili kuwawezesha viongozi hao, ambao mto huo unapita katika maeneo yao kuona kwa macho yao ulivyokauka, waweze kuchukua hatua za haraka kuunusuru.

Baada ya kuona hali hiyo, viongozi hao walikubaliana kuchukua hatua za haraka, kuurejesha mto huo katika hali yake ya kawaida kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika na wadau wengine wa maji.

SABABU ZA KUKAUKA
Mhaidrolojia wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Grace Chitanda, anasema  kuanzia miaka ya 1994, Mto Ruaha Mkuu umekuwa ukikauka katika eneo la kilomita 120 ndani ya wilaya ya Iringa pekee kila mwaka.

Mto huo anasema, kwa kiasi kikubwa umeathiriwa na matumizi makubwa ya maji kwa ajili ya shughuli za kilimo, kuingizwa mifugo kwa wingi hasa katika maeneo chepechepe, matumizi ya viwanda, uchimbaji madini na makazi katika vyanzo vya maji kiasi cha kuharibu mkondo wa mto na mabwawa.

Pia anasema upandaji wa aina za miti ambazo hazihifadhi maji na uendeshaji wa mitambo ya umeme usiozingatia hifadhi ya mazingira kutoka katika mabwawa yanayohifadhi maji, kunahatarisha viumbe hai na ikolojia ya mto huo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Maji wa WWF, Kevin Robert, anasema mto huo unakauka kutokana na mchanga kujaa hivyo maji kupoteza mwelekeo kwa kutopita katika mkondo wake wa asili, hivyo mengi hupotelea njiani.

Pia anasema ufugaji  holela wa kuhamahama katika eneo hilo hasa katika Mto Ruaha Mkuu ( mifugo iliyohama kutoka Ihefu bado inazagaa katika maeneo ya vyanzo vingine vya maji ndani ya bonde hilo ). Anataja tatizo jingine ni uchepuaji wa mifereji unaosababisha mito kuhamahama na wakati mwingine maji kutuama, kuzagaa na kutengeneza matindiga.

ATHARI ZA KUKAUKA RUAHA MKUU
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Dk. Chris Timbuka, anataja baadhi ya athari za kukauka kwa mto huo kuwa ni, binadamu na wanyama kukosa maji, kupungua kwa watalii katika hifadhi hiyo hivyo kulikosesha taifa fedha za kigeni, mivutano ya kugombea maji, kilimo kudumaa, uzalishaji umeme kupungua, wanyama kuvamia makazi ya watu maeneo ya jirani kwa ajili ya kutafuta maji na wanyama kufa.

Mratibu wa Maji wa WWF, Robert, anasema kukauka kwa mto huo kunatishia si tu uhai wa wanyama na ikolojia ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, bali pia wananchi  wanaotegemea maji ya mto huo kuendesha shughuli zao za kiuchumi, ikiwamo kilimo na uvuvi, kusababisha migogoro ya kugombania rasilimali ndogo ya maji na kushusha uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera, Kidatu na Kihansi yanayotegemea kwa kiasi kikubwa maji ya mto huo.

WANYAMA HATARINI
Athari iliyodhahiri utakayoiona unapotembea mto huo katika Hifadhi ya Ruaha ni kuathirika kwa kiasi kikubwa kwa viumbe hai, ambao maisha yao yanategemea maji ya mto huo, jinsi wanavyohangaika kutafuta maji.

Katika Hifadhi ya Ruaha, ambayo inaelezwa kuwa, na tembo wengi zaidi ya 25,000 kuliko mbuga yoyote ya wanyama nchini, mwandishi wa makala haya ameshuhudia makundi ya wanyama hao yakihangaika kutafuta maji ya kunywa na kuoga  ili kupoza miili yao na wengine wakichimba ardhi, katika maeneo tambarare na chepechepe ili kupata maji yaliyo chini ya ardhi kuokoa uhai wao.

Wakati jitihada za serikali na wadau wengine zikielekezwa zaidi kupambana na ujangili, unaelezwa kuwa tishio kubwa linaloweza kusababisha wanyama hao kutoweka kabisa. Tatizo hili la kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu  linaloonekana kutopewa uzito mkubwa kukabiliana nalo, linawaweka wanyama hawa adimu katika hatari nyingine ya kupoteza uhai kwa wingi sababu ya kukosa maji.

Viumbe wengine ambao maisha yao kwa kiasi kikubwa yanategemea maji ya mto huo ni kama viboko, mamba, samaki na mengine, maisha yao nayo yapo hatarini endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuurejesha mto huo katika hali yake ya asili na kuyafanya maji kutiririka katika kipindi cha mwaka mzima.

KILIMO CHA ATHIRIKA

Mhaidrolojia Chitanda, anasema zaidi ya hekari 10,5000 hulimwa kwa sasa, katika eneo hilo kwa kutegemea maji ya Mto Ruaha Mkuu, ambao ujazo wake wakati upo sawa ulikuwa meta 20,000 lakini kwa sasa umeshuka hadi kufikia chini ya meta 1,000.

Kutokana na mto huo kukauka, shughuli za kilimo za wakulima hao ambao wengi wao hutumia maji ya mto huo kumwagilia mashamba yao, zimeathirika na kushusha uzalishaji wa mazao.

Pia kuna wakulima wakubwa wawekezaji wa mashamba ya Kapunga wilayani Mbarari, mkoa wa Mbeya, ambao wanategea maji ya mto huo kwa ajili ya mashamba yao.

MGAWO WA UMEME 
Eneo hili lina mabwawa muhimu ya kuzalisha umeme ya Mtera lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya meta za ujazo milioni 3,600 (eneo 629 mm3), Kidatu meta za ujazo milioni 125 na Kihansi meta za ujazo milioni 1.0. 

Matumizi makubwa ya maji katika mabwawa haya, hasa la Mtera yakiambatana na hali ya ukame wa muda mrefu, yamesababisha maji kutumika chini ya kiwango kinachoruhusiwa‘Dead Storage’ na kupeleka mgawo wa umeme, ambao una athari kubwa ikiwamo kushusha uzalishaji viwandani, kuzorotesha shughuli za ujasiriamali na kupandisha gharama za maisha nchini.

Hali hii kama itaendelea, kuna uwezekano mkubwa mgawo wa umeme ambao ulitikisha taifa miaka ya karibuni na kuathiri shughuli za kiuchumi kurudi tena.

WANASIASA LAWAMANI
Wanasiasa wanalaumiwa kuwa, moja ya sababu za mto huo kuathirika kutokana na kuwatetea watu wanaosababisha uharibifu huo kwa manufaa yao ya kisiasa, hasa kupata kura toka kwa wananchi hao wakati wa chaguzi.

HATUA ZA KUCHUKUA
Ni wazi kuwa, Mto Ruaha Mkuu upo hatarini kukauka kabisa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, zinahitajika nguvu za pamoja za wadau wote, ikiwamo serikali, mamlaka zinahusika na uhifadhi na maji kama vile Bodi ya Maji ya Bonde la Mto Rufiji, WWP na wananchi wa maeneo husika kukabiliana na tatizo hili.

Kati ya hatua za haraka zinazoweza kuchukuliwa ni, uundaji wa kamati za kusaidia usimamizi wa matumizi ya maji ya mto huo, kudhibiti na kusimamia matumizi ya maji ya umwagiliaji na uzalishaji umeme na kuhamasisha wananchi na kuwapa elimu ya matumizi bora ya maji na mazingira.

Nyingine ni kuimarisha vyama au jumuiya za watumiaji maji, ambazo kwa sasa zipo 33 na kuwaondoa wavamizi na wakaaji katika maeneo ya vyanzo vya maji, ikiwamo mifugo iliyovamia maeneo ya mto na chepechepe na kuondoa michanga iliyojaa katika maeneo ya mto, ili maji yaweze kutiririka vizuri katika mkondo wake wa asili kwa kipindi chote cha mwaka kama ilivyo kuwa zamani.

CHANZO: NIPASHE
http://www.ripoti.com/openx/www/delivery/lg.php?bannerid=647&campaignid=424&zoneid=267&loc=1&referer=http%3A%2F%2Fwww.ippmedia.com%2Ffrontend%2Findex.php%3Fl%3D78097&cb=937eec3fd3
Habari Zaidi


No comments:

Post a Comment