Monday, February 2, 2015

Mwenyekiti wa kijiji jela miaka 20 kwa ujangili




Posted  Jumatatu,Februari2  2015  saa 12:14 PM
Kwa ufupi
Ujangili wa meno ya tembo umeiharibu taswira ya Tanzania kimataifa ambapo mwaka jana Shirika la Kimazingira la EIA lilitoa ripoti iliyoonyesha kukithiri kwa ujangili.
Rufiji. Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgomba, Kata ya Mgomba, Jumanne Ligonge amehukumiwa jela miaka 20 au kulipa faini ya Sh49.1 milioni baada ya kupatikana na vipande 43 vya meno ya tembo kinyume cha sheria.
Ligonge aliyeshinda kiti hicho katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka jana mwishoni kupitia Cuf, alikamatwa na polisi akiwa amepakia vipande hivyo kwenye pikipiki.
Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Rufiji, Stuart Sanga alimtia hatiani mtuhumiwa baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Mtuhumiwa alidai kuwa siku ya tukio hakuwa na vipande, hivyo bali alikuwa amembeba mgonjwa kutoka Nambunju Mbwara.
Hakimu Sanga alisema makosa ya watu kukutwa na nyara za Serikali yamekithiri na hukumu hiyo ni fundisho kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Polisi Josam Gabikwa alidai mahakamani hapo mbele ya Hakimu Muhidin Matitu (marehemu) kuwa Machi 30, mwaka jana, saa moja jioni eneo la Nyamwage, mtuhumiwa alikamatwa na meno ya tembo vipande 43 kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa alikana shtaka hilo na kesi ilianza kusikilizwa na hakimu Matitu, ambaye alipostaafu na baadaye kufariki dunia, kesi hiyo ilihamishiwa kwa hakimu Sanga aliyehamia hapo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.



No comments:

Post a Comment