Tuesday, December 17, 2013
Wabunge wataka Operesheni Kimbunga,Tokomeza Ujangili
NA JOHN NGUNGE
17th December 2013
Wasema ni muhimu kuendelea kufanyika
Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, imependekeza Serikali iendeleze Operesheni Tokomeza Ujangili na Operesheni Kimbunga ambazo zimesitishwa kwa muda.
Akisoma kwa niaba ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Anna Abdallah, Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa (CCM), alisema, operesheni hizo zililenga kutokomeza wahalifu na uhalifu nchini.
“Pamoja na dosari zilizojitokeza na ambazo tayari zinafanyiwa kazi na Serikali na Bunge, bado kamati inaishauri Serikali iendeleze operesheni hizo kwa lengo la kuwatokomeza majangili na kuwaondoa wageni wote walioingia nchini kinyume cha sheria,” alisema.
Alisema kamati yake inaamini kwamba operesheni hizo bado ni muhimu kuendelea kufanyika na kinachohitajika ni kurekebisha dosari zilizojitokeza na kusonga mbele.
Wananchi katika maeneo kadhaa nchini walizilalamikia operesheni hizo kuwa zilikuwa zinatelekezwa bila kufuata taratibu na kukiuka haki za binadamu.
Katika kikao cha Bunge cha 13, wabunge pia walilalamikia operesheni hizo kuwa inakwenda kinyume na haki za binadamu ikiwa ni pamoja na wananchi kuporwa mifugo na kuuawa.
Aliyekuwa wa kwanza kuchangia mjadala huo ni Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola (CCM) ambaye katika hitimisho lake alitoa hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kile ambacho alikiita kuwa ni unyanyasaji wa wafugaji na uporaji wa mifugo yao.
Profesa Msola alielekeza shutuma zake kwa Serikali kuwa ilifanya operesheni zake kwa pupa bila kufanya maandalizi hivyo kuwaathiri wananchi wasiokuwa na hatia.
Kufuatia malalamiko hayo, serikali iliamua kusitisha operesheni hizo kwa muda ili kufanya tathmini.
Novemba 7, mwaka huu, wakati Rais Jakaya Kikwete, akihutubia Taifa kupitia Bunge, alisema malalamiko ya wabunge dhidi ya kuwapo kwa ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na mifugo yenyewe, yatafanyiwa kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha wabunge hao kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.
Alisema hakukasirishwa na maoni ya Wabunge kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwani shabaha ya Operesheni hiyo ni kuokoa maliasili za misitu na wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia kutoweka kwa raslimali hizo kama Ndovu na Faru wanaokwisha.
Kuwarejesha makwao wahamiaji haramu
Kuhusu kuwarejesha makwao wahamiaji haramu walio magerezani, Kamati hiyo ilisema: “Magereza yetu kwa sasa yanakabiliwa na msongamano mkubwa wa wafungwa, kati ya wafungwa hao wengine ni wahamiaji haramu ambao hukaa magerezani kwa muda mrefu bila ya kurudishwa makwao.”
Alisema kwa mfano, kamati ilipofanya ziara mkoani Mbeya ilikuta kulikuwa na jumla ya wahamiaji haramu 262 kwenye gereza la Ruanda.
“Kamati inashangazwa na Serikali kudai kuwa haina fedha za kuwarudisha wahamiaji haramu makwao wakati inatumia fedha nyingi kuwalisha na kuwatunza magerezani.
“Hivyo basi, kamati inahimiza Serikali iwarudishe makwao wahamiaji hao ili kupunguza mzigo kwa walipa kodi wa Tanzania kuendelea kuwatunza wahamiaji haramu wapatao 1,172 katika magereza yote,” alisema.
Kubadilishana wafungwa
Aidha, kamati ilitaka uwepo utaratibu wa kubadilishana wafungwa, kutoka nchi za nje waliofungwa kwa makosa mbalimbali ya jinai.
“Moja ya njia za kupunguza idadi ya wafungwa wa aina hiyo ni kwa serikali kuweka utaratibu wa kisheria wa kubadilishana wafungwa na nchi zenye wafungwa wengi kwenye magereza yetu, hasa nchi za jirani za Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya ili wakatumikie adhabu ya kifungo kwenye magereza ya nchini kwao,” alisema.
Maandamano yasiyo rasmi
Kamati imesema katika siku za karibuni umezuka mtindo wa vikundi vya watu, vyama vya kisiasa au mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya maandamano bila utaratibu wa kueleweka, yaani kufanya maandamano siku yo yote, mahali popote, na wakati wo wote, hivyo kusababisha usumbufu miongoni kwa jamii ikiwa ni pamoja na shughuli za kijamii kusimama.
“Kamati inatambua haki ya kikatiba ya vikundi mbalimbali kujumuika bila ya kuvunja sheria. Hata hivyo, ni maoni ya kamati kwamba serikali ipitie upya sheria zake ili hatimaye iandae muswada wa sheria itakayoweka utaratibu mahususi wa kuandamana utakaozingatia siku, muda na mahali ili kumwezesha mwananchi atumie haki yake ya kuandamana bila ya kuingilia uhuru wa mtu mwingine,” alisema.
Mitambo ya CCTV
Kamati hiyo imeishauri Serikali kuanzisha matumizi ya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya ulinzi katika maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya watu, na hasa matumizi ya kamera maalum (CCTV), ili kunasa nyendo za wahalifu katika maeneo hayo.
“Vile vile katika ukamataji wa madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, serikali kupitia Jeshi la Polisi linashauriwa ianzishe utaratibu wa kuweka kamera maalum zitakazowanasa madereva wote wanaovunja sheria za usalama barabarani.
“Kazi ya ukamataji makosa ya barabarani sasa itafanywa na kamera maalum zitakazoonyesha baadhi yao hutumia fursa hii kupokea rushwa,” alisema.
Msuguano wa mapato ya viza
Katika kutekeleza majukumu yake, Idara ya Uhamiaji, kamati imebaini kuwa kuna msuguano wa mapato ya viza kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwani hivi sasa Wizara ya Mambo ya Nje wameweka utaratibu wa kutokuwa na maofisa uhamiaji kwenye balozi nchi za nje na hivyo kusababisha shughuli za uhamiaji kufanywa na watu wasiokuwa na ujuzi huo, ikiwemo suala la ukusanyaji wa mapato ya viza.
Usalama ndani ya Bunge
Kamati imeshauri kanuni na sheria zote zinazohusiana na haki na madaraka ya bunge zipitiwe upya ili kuweka kanuni za maadili ya wabunge kwa lengo la kukabiliana na vitendo vinavyolidhalilisha bunge.
“Katika kikao cha Bunge cha 12 lilitokea tukio la aibu ndani ya Bunge ambapo baadhi ya wabunge walirushiana ngumi na mateke bungeni na askari wanaolinda usalama wa Bunge baada ya askari hao kutekeleza amri halali ya kiti na hivyo kuhatarisha hali ya usalama wa Bunge na wabunge.
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment