08/12/2013 | Posted by Mwandishi Wetu-Tanzania daima.
WAZIRI
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amesema Waafrika wakiwamo Watanzania wanapaswa
kujiandaa kunufaika na uvunaji mpya unaofanyika katika rasilimali zake.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mkutano wa biashara na vitega uchumi unaohusisha Tanzania
na Uingereza jana jijini London, alisema maliasili za Afrika bado hazijasaidia
sana maendeleo ya Waafrika kama ilivyo kwa mataifa mengine.
“Kutokana
na maendeleo ya biashara, maliasili nyingi zimekuwa zikutumika sehemu
mbalimbali duniani…ukilinganisha na bara la Afrika ambalo halina maendeleo
makubwa, maliasili nyingi zinahitajika kutumika kutokana na uwepo wake kwa
wingi,” alisema Sumaye.
Katika
hotuba yake iliyopatikana jijini Dar es Salaam jana, Sumaye alisema kuwepo kwa
maliasili hizo kunatoa mvuto kwa wengi kuliangalia kwa macho mawili bara la
Afrika, hivyo kuwafanya wengi kujitokeza kuziwania huku wenyeji wakijiuliza
kuhusu ni kwa namna gani watanufaika nazo.
Sumaye
ambaye amechukua nafasi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyeahirisha kushiriki
mkutano huo, alisema uvamizi unaofanyika sasa ni kama mwingine wowote
uliofanyika katika nyakati zilizopita.
Aliongeza
kuwa uvamizi wa sasa una sura tofauti, lakini swali la kujiuliza ni kuhusu nani
anayehofia uvamizi huo, kama ni raia wa kigeni au mwenyeji.
“Kwa mimi
uvamizi wa wawekezaji kama vile Wachina katika rasilimali zilizopo ni jambo
zuri na hasa kama Waafrika watanufaika na wataongoza mchakato wa matumizi ya
rasilimali hizo,” alisema.
Alifafanua
kuwa ujio wa wavamizi hao ni jambo zuri kwa kuwa wanafanya kwa ushindani, hivyo
kutoa nafasi nyingi za kupata mikataba minono, kutegemea na jinsi watakavyokuwa
wamechanga karata zao vizuri.
Sumaye
alisema jambo la msingi ni kuhakikisha wazalendo wanashirikishwa kwa wingi
kadiri iwezekanavyo, na hasa katika kupata fursa za ajira, teknolojia, ushuru
na ongezeko la thamani za rasilimali zao.
Mkutano
huo ulimhusisha Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter Kalaghe, maofisa
ubalozi, Watanzania waishio nje ya nchi na wageni wengine.
Hata
hivyo, Sumaye alionya kuwa jitihada za kuvutia wawekezaji haziwezi kufanikiwa
kama viongozi wake na serikali hazitakuwa makini katika vita dhidi ya vitendo
vya rushwa.
“Rushwa
katika mazingira yoyote, iwe kwa mwekezaji au serikali, haipaswi kuachiwa
iendelee kuwepo,” alisema Sumaye na kuongeza kuwa zipo baadhi ya sekta ambazo
zinaendelea kwa kasi kubwa kama ile ya utalii.
No comments:
Post a Comment