Friday, December 27, 2013

Utalii umeanza kunufaisha wazawa Z’bar


Na Theodatus Muchunguzi
27th December 2013

Hoteli ya Hideaway Nungwi Resort iliyoko katika ufukwe wa Nungwi, ambayo ni miongoni mwa hoteli zenye viwango vya juu duniani.
Baada ya uhasama wa kisiasa kuzuia maendeleo ya sekta mbalimbali visiwani Zanzibar, utalii umeanza kufufuka na mchango wake kwa uchumi wa visiwa vya Pemba na Unguja unaongezeka.

Inakadiriwa kuwa hivi sasa mchango wa sekta ya utalii kwa pato la Zanzibar umefikia asilimia 27 na kwamba asilimia 80 ya fedha zinazotokana na sekta hizo ni za kigeni.

Ongezeko la pato katika sekta hiyo linatokana na kuibuka kwa hoteli za kitalii, nyingi miongoni mwa hizo zimejengwa katika maeneo ya fukwe za bahari na wageni wanaofikia katika hoteli hizo idadi kubwa ni watalii kutoka mataifa tajiri duniani.

Unapotembelea maeneo hayo, kwa hakika huwezi kuamini kuwa upo Zanzibar, unaweza kufanya makosa kuamini kuwa siyo Pemba au Unguja kwa sababu ya uwingi wa wageni kutoka mataifa mbali mbali ya Ulaya na Marekani.

Kamisheni ya Utalii Zanzibar, inasema tangu kuanzishwa kwa sera ya kukaribisha vitega uchumi na sekta binafsi, asilimia 80 ya miradi iliyotekelezwa ni ya sekta ya hoteli na huduma za utalii za viwango mbalimbali.

Jumla ya hoteli 354, ikiwa ni pamoja na nyumba za kulaza wageni zenye vyumba 7,421 na vitanda 14,076 vimeshamiri visiwani Zanzibar, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa miji zikiwa na uwezo wa kuhudumia wageni 169,223 mwa mwaka 2012.

Sekta hii hivi sasa imetoa mchango wa ajira za moja kwa moja kwa vijana 13,017 na zaidi ya ajira 45,000 kwa zile nafasi zisizo na uhusiano wa moja kwa moja. Matarajio ni kwamba zaidi ya asilimia 50 ya waajiriwa Zanzibar watatokana na sekta ya utalii ifikapo mwaka 2020.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Watembeza Watalii Zanzibar (Zato), Hassan Ali Mzee, anatofautiana na takwimu za Kamisheni ua Utalii kwa kusema kuwa sekta ya utalii inatoa ajira za moja kwa moja 15,000 na zisizo za moja kwa moja 60,000.

Anaongeza kusema kuwa watalii wanasaidia kuongeza pato kwa kuwa mtalii mmoja analazimika kulipa Dola 95 anapoingia nchini, Dola 50 kwa ajili ya viza na Dola 45 kwa ajili ya kodi ya matembezi, chakula na hoteli.

Viongozi wa hoteli nyingi zinazomilikiwa na wageni wanasema kwamba hoteli hizo zimeweza kutoa ajira kwa wananchi wengi, hususani Wazanzibari na baadhi kutoka Tanzania Bara.

Kwa mfano, hoteli ya Hideaway Nungwi Resort iliyoanzishwa miezi saba iliyopita na miongoni mwa hoteli zenye viwango vya juu duniani, ina wafanyakazi takribani 250 huku wafanyakazi 200 wakiwa ni wa kutoka Zanzibar na wengine 50 wanatoka Tanzania Bara.

Hoteli nyingine ya Diamond Dream of Zanzibar ambayo nayo inasema ina imeajiri zaidi ya wafanyakazi 250, wafanyakazi takribani 190 mwanatoka Zanzibar na wengine kati ya 50 na 60 ni kutoka Tanzania Bara.

Ujenzi wa hoteli hizo umewakomboa wananchi kwa kuwapatia ajira ambazo zinawapatia kipato cha kukidhi mahitaji yao muhimu kwa maisha ya maisha yao ya kila siku.

Hata hivyo, hakuna mazuri yasiyo na kasoro. Pamoja na Watanzania kunufaika na ajira hizo, yako malalamiko kuwa nafasi za juu katika hoteli za kitalii zinashikiliwa na wageni huku wenyeji wakiishia kufanya kazi ndogo ndogo za kupika, kufua, kusafisha vyumba na bustani.

Raia wengi wa kigeni ambao wanatajwa kuwa wameajiriwa katika hoteli hizo na kushika nafasi za juu na kulipwa zaidi ni wa kutoka Kenya.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa wazawa wa Zanzibar na Watanzania bara wanakwama kupata ajira katika hoteli za kitalii kwa kukosa uelewa wa lugha pamoja na kufanya kazi kwa mazoea.

Kutokana na hali hiyo, watalii wanajikuta wanashindwa kupata huduma kwa usahihi kutokana na tatizo la mawasiliano baina yao na wahudumu.

Meneja wa mauzo na masoko wa Hideaway Nungwi Resort, George Kiruku, anasema kuwa moja ya changamoto zinazoikabili hoteli hiyo ni wafanyakazi wenyeji kutokuwa na uwezo wa lugha za kigeni na kwamba kwa hali wanawasiliana kwa matatizo na watalii wanaotoka nje ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Kiruku ambaye ni raia wa Kenya, anasema watalii wanahitaji huduma za viwango na kwamba kwa sasa wakilalamika kuwa huduma wanazopewa na wenyeji kwamba haziridhishi.

“Wageni (watalii) wanalalamikia kutohudumiwa kwa wakati. Mgeni anaweza kuagiza chakula, lakini akacheleweshewa,” anasema Kiruku.

Hata hivyo, Kiruku anasisitiza kwamba wengi waliopata nafasi za ajira katika hoteli hiyo ni wa maeneo jirani huku akiahidi kwamba mpango wa kuwasaidia vijana na kinamama wa eneo la Nungwi unaandaliwa.

Kwa upande wake, Meneja wa hoteli ya Diamond Dream of Zanzibar, Allan Ochner, anapozungumzia changamoto ya lugha, hususan Kiingereza kwa wafanyakazi wenyeji, anasema huko nyuma kulikuwapo na malalamiko hayo, lakini kadri wanavyopatiwa mafunzo wanafanya vizuri.

Ochner ambaye anatoka Mombasa, Kenya, anasema kwamba wafanyakazi wanaosikiliza na kufuata maelekezo pamoja na kupenda kujiendeleza wanapandishwa vyeo, lengo ikiwa ni kuwapa motisha wa kijiendeleza zaidi.

“Tunapima utendaji wao na wanaobainika kufuata maelekezo wanapandishwa. Sasa baadhi ya idara wanaziongoza wafanyakazi wa Zanzibar,” anasema.
Omar Ibrahim, msimamizi wa shamba la viungo la Kizimbani, anawashauri vijana kujiendeleza na kuchangamkia ajira zilizoko katika sekta ya utalii.

Anasema baada ya kujiendeleza, yeye na wenzake sasa wamepata sifa ya kuwa wanawatembeza na kuwahudumia watalii wanaofika katika mashamba yao ya viungo.

“Tujitahidi kusoma hata kama tumeshindwa shule tujiendeleze katika kozi mbalimbali,” anasema Ibrahim ambaye shamba lake na wanakijiji wenzake linazalisha pilipili manga, vanilla, hiliki, alovera, mrangirangi, majani ya chai na mdarasini.

Afisa Mipango wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Dk. Miraji Ukuti Ussi, anakiri kwamba lugha ni changamoto miongoni mwa wafanyakazi katika hoteli za kitalii, lakini anasema hatua kadhaa zinachukuliwa kukabiliana nayo.

Dk. Ussi anasema kuwa moja ya hatua hizo ni kuboreshwa na kupanuliwa kwa Chuo cha Utalii cha Maruhubi ili kutoa huduma zinazohitajika za utalii.
Baadhi ya hoteli za kitalii zinalalamika kwamba hali ya hewa ya Zanzibar haitabiriki, kiasi kwamba wakati mwingine inabadilika ghafla na kusababisha usumbufu katika shughuli za uzalishaji wa mboga mboga zinazopendwa na watalii wengi.

Ochner wa Diamond Dream of Zanzibar, ambayo ina uwezo wa kuhudumia watalii 200 kwa siku na kulipa kodi hadi Dola za Marekani 500,000 kwa mwaka anasema kuwa hali hiyo imekuwa ikiwakwaza na kushindwa kuzalisha mboga hizo.

Hata hivyo, Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kupitia kwa Ofisa wake wa Mipango, Dk. Miraji Ussi, anathibitisha kuwapo kwa malalamiko hayo, lakini anasema kuwa kuna mpango unaotekelezwa wa kuihamasisha Mamlaka ya Kutangaza Vitega Uchumi Zanzibar (Zipa) na wananchi kujihusisha na uzalishaji wa kilimo cha kisasa.

Anasema kuwa mpango huo ulianza baada ya baadhi ya hoteli kusema kuwa hali ya hewa wakati mwingine inakwaza uzalishaji wa baadhi ya mahitaji ya vyakula.

Mashamba ya viungo:
Uzalishaji wa viungo ni fursa nyingine muhimu kwa sekta ya utalii Unguja ambako kuna mashamba katika maeneo ya Kijichi na Kizimbani katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

Shamba la Kijichi ambalo lina ukubwa wa ekari nne linamilikiwa na wanakijiji wapatao 300 na limewawezesha kuwapa ajira vijana kadhaa wanaolihudumia na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao.

Omar Ibrahim, ni mmoja wa vijana hao anayesema watalii wengi wanapenda kutembelea shamba hilo kujionea na kununua aina kadhaa ya viungo kama pilipili manga, majani ya chai, binzari, vanilla, mdarasini, hiliki, mrangirangi na alovera na kuwaachia fedha.

“Tunapata fursa za kazi za vibarua na kupata fedha nyingine tunazoachiwa na watalii baada ya kuwapa huduma nzuri. Vijana wasio na ajira waje tushirikiane,” anasema Ibrahim ambaye hata hivyo anasita kueleza kiasi halisi cha fedha wanazopata kwa siku kutoka kwa watalii.


Hifadhi ya Jozani:
Hifadhi ya Taifa ya Jozani Chwaka Bay iliyoko katika wilaya za Kati na Kusini katika Mkoa wa Kusini Unguja, ni kivutio kingine kikubwa cha utalii Zanzibar.
Hifadhi hiyo ya miti ya asili yenye ukubwa wa hekta 5,000 ni sehemu inayovutia watalii wengi kwenda pamoja na watafiti kupita kufanya tafiti zao.

Kivutio kikubwa zaidi katika hifadhi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004 ni kuwa na kima mwekundu pekee duniani, ambaye pia anafahamika kwa jina la Punju kutokana na sumu aliyonayo.

Inasemekana kwamba mbwa au mnyama yeyote akila nyama yake, ananyonyoka manyoya. Hifadhi hiyo pia inahifadhi paa nunga ambaye pia ni adimu.
Ali Ally Mwinyi, Ofisa wa Idara ya Misitu ambaye pia ni Meneja wa Uhifadhi Ghuba ya Chwaka, anasema kiasi cha Sh. milioni 180 zinalipwa na watalii takribani 24,000 kwa mwaka wanaoingia katika hifadhi hiyo.

Mwinyi anasema kuwa nusu ya mapato yatokanayo na hifadhi hiyo yanabakia katika jamii ya wanavijiji vinavyozungukwa na hifadhi na kiasi kinachobaki kinakwenda serikalini.
Rais Shein anasemaje kuhusu utalii?

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, anapozungumzia utalii, anasema Serikali ya awamu ya saba, iliingia madarakani ikiwa na dhamira kubwa ya kuimarisha sekta ya utalii na kwamba lengo ni kuibadilisha sura ya sekta hiyo ili iweze kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa taifa.

Dk Shein anasema angependa kuona utalii unakuwa sekta kiongozi ili iweze kuwa kichocheo cha sekta nyingine.

Anasema Kamati za Utalii kwa Wilaya za Unguja na Pemba tayari zimeundwa ili kuziimarisha huduma za utalii kwenye Wilaya, na kuwahamasisha wananchi kuendeleza miradi ya uzalishaji mali, hususan kilimo cha mboga mboga, matunda, biashara ndogo ndogo na kadhalika.

Chuo cha Maendeleo ya Utalii kilichoko Maruhubi hivi sasa kinaimarishwa ili kitekeleze kwa ufanisi zaidi lengo la kujenga rasilimali watu wenye ujuzi, utaalamu na stadi zinazohitajika.

“Lengo letu ni kukifanya chuo hicho kiendelee kutoa mafunzo ya utalii unaotilia maanani, mila, utamaduni na desturi zetu pamoja na hifadhi ya mazingira. Hivi sasa Serikali ishachukua hatua ya kuibua maeneo mapya ya vivutio vya utalii yakiwamo mapango, michezo ya asili, matamasha, maeneo ya hifadhi ya wanyama,” anasema na kuongeza:

“Hatua zinachukuliwa za kuimarisha utalii wa kumbukumbu za kihistoria kwa maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba, kuimarisha utalii wa kiutamaduni na kuuendeleza utalii wa ndani wenye kuyatunza mazingira.”

Rais Shein anasema juhudi za pamoja zinazochukuliwa na serikali na sekta binafsi zimepelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii kututembelea Zanzibar. Katika mwaka 2011 Zanzibar ilipokea watalii wapatao 175,067 na mwaka 2012 watalii 169,223 walifika nchini.  
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment