Saturday, December 7, 2013

Ujangili unapoteza ubora wa hifadhi’




 TEMBO NI MIONGONI MWA WANYAMA WAKUBWA(BIG FIVE)WALIOKO  HATARINI KUTOWEKA KATIKA HIFADHI ZA TAIFA NA MAPORI YA AKIBA NA HIYO INACHANGIA KUPOTEZA UBORA WA UHIFADHI-PICHA NA JOURNO TOURISM

Posted by



WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema wimbi la ujangili wa kutisha lililozuka hivi karibuni la kuua wanyama hususan faru na tembo linaelekea kutishia uhai wa wanyamapori na kupoteza ubora wa hifadhi nchini.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi baada ya kuhitimisha mbio za Serengeti zilizokuwa maalumu kwa ajili ya kupinga ujangili katika hifadhi mbalimbali za taifa.
Akisoma hotuba ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Paschal Mabiti, alisema hivi karibuni kumezuka wimbi la ujangili kwa kiwango cha kusikitisha likihusisha wananchi wageni.
Alisema utalii ndiyo sekta inayoongoza kwa kulipatia taifa fedha za kigeni ambazo ndizo zinatumika kujenga barabara, hospitali, vyuo, viwanja vya ndege na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za serikali, hivyo alimtaka kila mmoja kusimamia na hata kushirikiana katika utoaji wa taarifa wa mauaji hayo.
“Ufanisi wa utalii unategemea sana uwepo wa wanyamapori, hasa kundi la wanyama wanaoitwa ‘big five’ linalohusisha tembo, faru, simba, nyati na chui, hivyo si vema wakaendelea kuachwa wakiteketea,” alisema Mabiti.
Alisema Mkoa wa Simiyu una kilomita za mraba 23,807.7 kati ya hizo 11,723.6 ni eneo la hifadhi ya mbuga za taifa ya Serengeti na mapori ya akiba ya Maswa, hivyo alisisitiza dhana ya kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori kwa kutumia shughuli mbalimbali za matamasha kama ilivyotumika mbio za Serengeti.
Mkurugenzi wa Kituo cha Michezo cha Serengeti, Dk. Titus Kamani, alisema ni wajibu kwa kila mwana Simiyu kutunza mazingira, kulinda wanyama, kupinga mauaji ya albino, ili waweze kuendelea kiuchumi wakiwa na amani.
Alisema suala la ujangili ni kubwa, hivyo si la kuachia serikali pekee ikafanya kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment