Dk.Emmanuel Nchimbi.
Na Daniel Mjema na Sharon Sauwa Mwananchi
Posted Decemba21 2013 saa 8:59 AM
Posted Decemba21 2013 saa 8:59 AM
Kwa ufupi
- Serikali kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kimahakama kuchunguza waliohusika na unyama wakati wa operesheni
Related Stories
Dar es Salaam / Dodoma. Ripoti ya Kamati ya Maliasili,
Ardhi na Mazingira iliyowasilishwa jana asubuhi bungeni mjini Dodoma,
imewang’oa madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilishindwa kusimamia
vizuri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni jana usiku na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani kwa matibabu.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Waziri wa kwanza kutangaza kujiuzulu alikuwa ni Kagasheki huku uamuzi wa mawaziri watatu kujiuzulu ukitangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kagasheki alitangaza kujivua wadhifa huo sa 2:09 usiku alipokuwa akichangia majumuisho ya ripoti ya kamati hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa kamati hiyo James Lembeli ambaye ni Mbunge wa Kahama (CCM).
Katika maelezo yake Kagasheki alisema: “…Mimi ni mtu mzima nimesikia hisia nzito sana kwa waliyoyasema wabunge. Rais Kikwete aliponiteua ilikuwa ni kwa furaha yake na operesheni hii, yaliyotokea yametokea hali ya wanyama huko si nzuri;
Mimi mwenyewe nimewasikia na nachukua fursa hii kuteremka ngazi hii ya uwaziri na nitachukua taratibu za kawaida kuijulisha sehemu inayohusika(Rais).
Baada ya Kagasheki kutangaza hatua hiyo, Spika aliwaita mawaziri Dk Nchimbi na Nahodha kuchangia hoja hiyo, hata hivyo hawakuwepo ndipo alipoitwa Dk Mathayo na kutoa maelezo yake.
Katika maelezo yake Dk Mathayo alisema kuwa ripoti hiyo haikumtendea haki kwani kamati ya Lembeli haikumwita kumhoji na kwamba hata ripoti nzima haikueleza kuhusika na kashfa hiyo. Hata hivyo akihitimisha hoja hiyo Lembeli alisema Dk Mathayo ameshindwa kusimamia mapendekezo tisa, yakiwemo matatizo ya wafugaji aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete Januari 18, 2006 alipoteuliwa kushika nafasi hiyo.
Akitoa maelezo ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mawaziri hao, Waziri Mkuu Pinda alisema: “Niliona nimtafute mkuu wa nchi (Rais Jakaya Kikwete), nilimpa picha yote ya kinachoendelea, alikubali ushauri wa Bunge; ..amekubali kuchukua ya uamuzi wa kutengua uteuzi wao(mawaziri).”
Akihitimisha mjadala huo wa ripoti ya kamati yake, Lembeli alisema: “...Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii nao wawajibishwe kutokana na kuhusika kwao na unyama uliotokea kwenye mpango wa Operesheni Tokomeza Ujangili. Rushwa iliyopo ndani ya wizara hiyo ni kubwa inakusanywa kwa kutumia simu, hivyo Serikali izichunguze simu zao kuanzia leo.”
Michango ya wabunge
Awali
hali ya hewa ndani ya kumbi wa Bunge jana ilichafuka baada ya wabunge kuchangia
kwa hisia kali, wakitaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kujiuzulu sambamba na
mawaziri wengine watatu.
Mawaziri
wanaotakiwa kujiuzulu ni wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha.
Mbunge wa
Longido, Lekule Laizer (CCM), alienda mbali zaidi na kutaka Bunge livunjwe
endapo Waziri Mkuu na mawaziri hao watatu watakataa kujiuzulu kwa lengo la
kung’ang’ania madaraka.
Michango
ya wabunge hao ilitokana na ripoti ya kamati ndogo ya uchunguzi ya Kamati ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake, James Lembele
iliyowasilishwa bungeni jana.
Ripoti
hiyo inayohusu Operesheni Tokomeza Ujangili (OTU), ilibainisha kuwapo mauaji ya
watu 13 na askari sita, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa, ubakaji, rushwa na
uporaji wa mali za wananchi.
Hata
hivyo pamoja na kamati ya Lembeli kumtaka Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Dk Mathayo David apime kama bado anastahili kuongoza wizara hiyo,
wabunge walimsafisha.
Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema), alisema hakuna jinsi ya kuonyesha
namna wabunge walivyokasirishwa na vitendo hivyo zaidi ya Serikali nzima kwa
maana ya Pinda kujiuzulu.
“Naomba
Waziri Mkuu uchukue ‘political responsibility’ (uwajibikaji wa kisiasa) na siyo
kwamba kwa kufanya hivyo anahusika la hasha… Kama hachukui hatua Bunge libebe
dhamana hiyo,” alisema.
Mbunge wa
kuteuliwa, James Mbatia alisema ripoti hiyo ya Lembeli imetaja kuwapo baadhi ya
wabunge wanaotuhumiwa kwa ujangili na kuhujumu OUT akitaka kamati iwataje ndani
ya Bunge.
“Bungeni
kazi yetu, sisi Wabunge ni kuisimamia Serikali kwa hiyo wale wabunge waliotajwa
kwenye ripoti watajwe ili nao wawajibike ili Bunge letu liwe na nia thabiti ya
kuisimamia Serikali,” alisema Mbatia.
Wabunge
waliochafua zaidi hali ya hewa kutokana na michango yao ya hisia kali dhidi ya
Pinda ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), na Mbunge wa Iringa Mjini
(Chadema), Mchungaji Peter Msigwa.
Lugola
alisema makosa ya operesheni hiyo yalianza mapema wakati operesheni ya kijeshi
ilipopelekwa kwa raia na kusema; “Hainiingii akilini kwamba aliyekuwa ana
command (kutoa amri) ni mwanajeshi.”
Wakati
operesheni hii ikitokea wanawake wanabakwa na watu wawili…Watu wameteswa,
mwanaume mwenzetu amelazimishwa kufanya mapenzi na mti Waziri Mkuu ulikuwa wapi
haya yakitokea?” alihoji.
Lugola
aliongeza; ”Kwa utaratibu wa nchi yetu tumekupa kila aina ya usafiri kuanzia
helikopta, ving’ora kila wakati vinalia ulikuwa wapi Waziri Mkuu wakati mambo
haya machafu yanatokea?”
Alisema
Vuai hawezi kupona katika suala hilo kwa kuwa wanajeshi ndiyo waliobaka, kuua
na kujeruhi na ndiyo walioua mifugo kwa risasi na kwamba atapona katika Bunge
hilo mbele ya haki hatapona. Vivyo hivyo alisema Dk Nchimbi hawezi kupona
katika kashfa hiyo kwa vile askari polisi ndiyo walioua, kubaka, kuwapa watu
vile na kuua mifugo akisema; ”Utaponea wapi Dk Nchimbi?”
Lugola
alisema pamoja na ripoti ya kamati kumnukuu Kagasheki akidai alinyang’anywa
mamlaka yote katika utekelezaji wa OTU, akihoji ni waziri wa namna gani
aendelee kukalia kiti cha uwaziri.
“Nimeisoma
ripoti hii hakuna mahali Dk Mathayo alipohusika anataka kutolewa kafara… Mifugo
yake imeuliwa hahusiki na sera yeye anahusika na wafugaji waliouawa pamoja na
mifugo,” alisema Lugola.
Hata
hivyo Lugola alisema Dk Mathayo anahusika na uzembe kwa kuwa wafugaji imeuawa,
mifugo imeuawa na kuhoji waziri huyo alikuwa wapi wakati hayo yakitokea ndani
ya Tanzania.
“Naendelea
kumshauri Rais kama tunaitakia mema nchi hii na kama tunataka CCM kiendelee
kuaminiwa na Watanzania, Rais amfukuze Waziri Mkuu mara moja,” alisisitiza
mbunge huyo.
Aliongeza
kusema; “vv Mawaziri wake hao hawawezi
kukwepa hili, watu wanachukua ‘political responsibility’ kwani Maige (Ezekiel)
alichukua Twiga porini?” alihoji na kuongeza kusema;
“Kama
tunataka tuwe na Bunge lenye viwango, Bunge lisilokuwa na ‘double standard’ (upendeleo)
na nyinyi watu wameua watu na nyinyi lazima muondoke ndiyo tutajenga heshima ya
nchi hii,” alisema.
Lugola
alenda mbali na kusema endapo Rais atashindwa kumfukuza Pinda katika wadhifa
wake huo, yeye atakuwa wa kwanza kupeleka hoja bungeni ili wabunge wapige kura
ya kumng’oa Waziri Mkuu.
Kwa
upande wake, Msigwa alisema wabunge wanapopendekeza Waziri Mkuu aachie ngazi
hawana chuki naye, lakini kwa madudu yaliyotokea chini ya usimamizi wake ni
lazima awajibike.
“Na kama
mnatuheshimu, mheshimiwa Waziri Mkuu ungekuwa unatayarisha makaratasi saa hizi
unaandika barua za kujiuzulu, tukufanyie sherehe ya kukuaga na nyie wa chini
yake mfuate,” alisema.
Msigwa
alienda mbali zaidi na kumnyooshea kidole Vuai kwamba ana rekodi mbaya kuanzia
Zanzibar na kwamba dhambi ya damu ya mauaji ya raia huko Pemba inamlilia na
kumfuata hadi Bara.
“Hata
sisi tunasema hamkuhusika ‘direct’ (moja kwa moja) lakini hapa tunazungumzia
uhai wa watu na watu waliokufa siyo wanachama wa CCM wala wa vyama vya
upinzani…Tutangulize utaifa,” alisema.
Mbunge
huyo alisema siku zote cheo ni dhamana na kwamba wasingependa Chadema
itakapochukua nchi iwapeleke mawaziri hao Mahakama ya Kimataifa ya Jinai,
iliyopo The Heague nchini Uholanzi, kwa kuwa hawatapona.
Lekule
ndiye aliyepigilia msumari wa mwisho aliposema endapo Bunge litamaliza mkutano
wake huo bila kuwapo mawaziri watakaowajibika, basi Rais alivunje Bunge ili
ufanyike uchaguzi mwingine.
No comments:
Post a Comment