Thursday, December 12, 2013

Matajiri waonywa kujihusisha na ujangili


12/12/2013 | Posted by Gordon Kalulunga | -Tanzania daima

MATAJIRI nchini wametakiwa kuacha kuwatumia vijana kujihusisha na ujangili kwenye hifadhi za taifa.
Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Hifadhi ya Kitulo, Pius Mzimbe, alipozungumza na Tanzania Daima katika Kijiji cha Ifupa, Kata ya Ilungu Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Mzimbe alisema kuna ujangili uliokuwa ukiendelea na unaoendelea katika hifadhi hiyo, ambao kimsingi matajiri ndio wanaojihusisha kwa kuwatumia vijana.
“Vijana wengi walikuwa wakitumika katika shughuli za ujangili, lakini kwa sasa baada ya kuwapa elimu ya kutunza mazingira na hifadhi ya kituo, vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa,’’ alisema Mzimbe.
Alieleza ujangili uliokuwa ukifanywa katika hifadhi hiyo ni uchimbaji wa viazi vya asili aina ya chikanda vinavyoota katika hifadhi hiyo.
“Viazi hivi vina soko Zambia ambako debe moja linakadiriwa kufikia sh 70,000 na watu wanaokula viazi hivyo ni matajiri na hapa Tanzania bado haijajulikana matumizi yake,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk. Norman Sigalla, alisema uongozi wa hifadhi hiyo umefanya vema kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa wananchi, hasa vijana.
“Ni jambo jema na sasa naamini pia kuwa imewapa fursa vijana kufahamiana katika kata nzima na kuwa na ujirani mwema,’’ alisema Dk. Sigalla.
Diwani wa Ilungu, Hashimu Mwashang’ombe, alisema awali wananchi wengi hawakutambua umuhimu wa kushirikiana na uongozi wa hifadhi, lakini baada ya kupata elimu na serikali kuonyesha mipaka kati ya wananchi na hifadhi, kwa sasa wananchi hawana tatizo na uongozi wa hifadhi.












No comments:

Post a Comment