WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII BALOZI KHAMISI KAGASHEKI
Na Sharon Sauwa na Habel Chidawali,Mwananchi
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Oktoba30 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini
wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika
mikoa inayopakana na Mbuga ya Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili,
lakini hatujasikia hao wakichukuliwa hatua,”
Dodoma. Wabunge jana walichachamaa na kushinikiza kutolewa kwa orodha ya vigogo
wanaojihusisha na ujangili wakati wa kikao cha kwanza cha mkutano wa 13 wa
Bunge unaofanyika mjini Dodoma.
Wabunge hao walitaka kutajwa kwa majina ya mawaziri, viongozi wa
Serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara hiyo.
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Mwibara
(CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo, akiitaka Serikali kuwataja hadharani na
kuwachukulia hatua viongozi wake na wanasiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge,
ambao wanatajwa kuhusika na vitendo vya ujangili nchini.
Lugola aliomba mwongozo wa Naibu Spika baada ya kutoridhishwa na jibu
lililotolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli.
Katika jibu hilo, Nyalandu alilieleza Bunge kuwa Operesheni Tokomeza
inayolenga kukomesha vitendo vya ujangili nchini bado inaendelea, lakini
alishindwa kulieleza Bunge ni nani hasa wamebainika kuhusika na vitendo hivyo.
Lugola, hata hivyo, aliitaka Serikali kuwasilisha ripoti bungeni
kuhusiana na utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Tangu Aprili tumekuwa tukipewa majibu mepesi kuhusiana na operesheni
hii, wakati suala hili si la masihara,” alionya Lugola.
Lugola alisema kuwa taarifa zimewataja watu wanaohusika na vitendo hivyo
wakiwamo viongozi serikalini, mawaziri pamoja na wabunge, lakini tangu
operesheni hiyo ilipoanza hakuna yeyote miongoni mwa hao wanaotajwa ambaye amekamatwa
isipokuwa wananchi wa kawaida.
Alisema operesheni hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa unyama kwani
wanaokamatwa hupigwa na kuteswa bila ya ushahidi unaoonyesha kuhusika kwao na
vitendo vya ujangili.
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini
wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika
mikoa inayopakana na Mbuga ya Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili,
lakini hatujasikia hao wakichukuliwa hatua,” alisema.
Kabla ya Naibu Spika kutoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Lugola,
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi, alisimama na kukiri kuwapo kwa vitendo vya utesaji wa watu wanaokamatwa
katika operesheni hiyo.
Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa msaidizi wake jimboni ambaye
alipigwa na kuteswa na askari hao kabla ya kuachiwa baada ya kushikiliwa kwa
siku moja, huku akionyesha kuwa ushahidi wa tukio hilo anao kwenye simu yake.
“Lakini sisemi haya kwa kutaka
kuitetea Serikali kuwa isilete ripoti hapa bungeni. Nadhani kuwa kuleta ripoti
hivi sasa haitakuwa vizuri. Ni vizuri tusubiri mpaka kazi hii ikamilike na nina
uhakika kuwa Wizara itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwenye kamati husika,”
alisema na kuongeza:“Nadhani kuwa `entry point’ (mahali pa kuanzia) yetu iwe ni kwenye ripoti hii itakayowasilishwa kwenye Kamati,”
Suala la ujangili limeingizwa bungeni wakati kukiwa na usiri mkubwa wa nani anahusika na vitendo hivyo, huku majina ya vigogo wanaotajwa kuhusika nayo wakiwa hawafahamiki.
Polisi watajwa vinara
Awali akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile, Nyalandu alisema Jeshi la Polisi ni vinara miongoni mwa makundi manne ya majeshi ambayo watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili.
Katika matukio saba ya ujangili yaliyowahusisha watumishi tisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, Nyalandu alisema kati ya hao sita ni polisi wakati kwa kupande wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza alikamatwa mtu mmoja mmoja.
“Katika matukio hayo, jumla ya meno ya tembo 686 na vipande 447 vikiwa na uzito wa kilogramu 4,253.9 vilikamatwa, jambo ambalo linaonyesha ukubwa wa tatizo hilo kwa vyombo vya ulinzi,” alisema Nyalandu.
Katika swali la msingi, Dk Ndugulile alitaka kufahamu idadi ya matukio ya upatikanaji wa pembe za ndovu yaliyohusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Katika swali la nyongeza, Lembeli ambaye ndiye aliyeuliza swali hilo kwa niaba ya Dk Ndugulile, aliitaka Serikali kuacha kigugumizi na kueleza ukweli kuwa wapo baadhi ya viongozi, wakiwamo wabunge ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo.
“Katika biashara ile kuna hali ya kulindana sana, hebu Serikali itueleze taarifa za kuwa wahusika wengine ni wanasiasa na baadhi ya wabunge, ukweli uko wapi, na kuna taarifa kuwa viongozi wa Polisi wanaoishi kuzunguka hifadhi zetu ndio ambao wanatumiwa kusafirisha nyara hizo, Serikali inasemaje?” alihoji Lembeli.
Nyalandu alisema Tanzania iko katika hali mbaya katika kiwango cha mauaji ya tembo ambapo wastani unaonyesha kuwa kila siku tembo 30 huuawa na majangili.
“Hata hivyo, suala la ulinzi bado tuko nyuma sana kwani wastani wa ulinzi wa kimataifa ni askari mmoja kwa kilomita za mraba 25, lakini sisi askari wetu mmoja analinda kilomita za mraba 150 ndani ya hifadhi,” alisema Nyalandu.
Serikali yakiri tatizo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha
akizungumza bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu, alikiri kuwapo fununu za
wanasiasa ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo na kusema Serikali
italifanyia kazi jambo hilo.
Nahodha aliwataka Watanzania kuwa watulivu wakati vyombo vya Ulinzi na
Usalama vinaposhughulika na kusafisha tatizo hili na kuonya wanasiasa kuacha
kutoa shinikizo kwa kutumia nguvu zao za kisiasa.
No comments:
Post a Comment