Thursday, October 31, 2013

Migogoro ya wafugaji yatikisa Bunge

 chanzo-Tanzania daima

WABUNGE wawili jana walitaka Bunge liahirishe shughuli zake ili lijadili migogoro kati ya wafugaji inayoendelea nchini pamoja na malalamiko kuhusu Operesheni Tokomeza Ufugaji Haramu na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Wabunge hao; Said Nkumba (Sikonge) na Kangi Lugola (Mwibara) walitaka wabunge wajadili jambo la dharura kuhusu migogoro ya wafugaji inayoendelea nchini.
Mbali na migogoro hiyo walitaka pia operesheni hizo zijadiliwe na wabunge kwa kuwa kwa sasa zinatumika kuwanyanyasa wafugaji na hali inayotishia machafuko kutokea nchini.
Alianza kusimama Nkumba baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu na kunukuu kanuni ya 47 (1, 2, 3) akitaka shughuli za Bunge zilizopangwa jana ziahirishwe, ili kujadili jambo hilo la dharura kuhusu migogoro ya wafugaji.
Alisema kwa sasa ipo migogoro ya aina tatu ambayo ni kati ya wafugaji na wakulima, wafugaji na wawekezaji na wafugaji na wahifadhi.
“Tatizo hili limekuwa kubwa kiasi cha kutishia uvunjifu wa amani hasa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro na Pwani.
“Na zaidi operesheni mbalimbali zinazoendelea kwa sasa zimesababisha uhasama na athari kubwa kwa wakulima na wafugaji kutokana na kupoteza mali zao, mifugo kuuawa na kupotea na vifo vya watu,” alisema.
Kwa upande wake, Lugola ambaye naye alilitaka Bunge kujadili migogoro hiyo, alisema hali ya wafugaji kwa sasa ni mbaya kutokana na operesheni hizo.
“Hivi ninavyozungumza ng’ombe 4,000 wamekamatwa kwa nguvu huko Kaliua na tayari ng’ombe 12 wameshachambuliwa kwa ajili ya kupigwa risasi kuwashinikiza wafugaji  walipe sh 180,000 kwa kila ng’ombe.
“Tusipojadili jambo hili mnada utaendeshwa na ng’ombe 4,000 watauzwa, ng’ombe wengine wanatumbukizwa kwenye madimbwi. Tatizo hili lisiposhughulikiwa litaleta machafuko makubwa hasa pembezoni mwa Serengeti,” alisema.
Hoja za wabunge wote hao ziliungwa mkono na wabunge.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kikanuni hoja hizo hazitakiwi kuungwa mkono.
“Hoja zote ni nzito haziwezi kudharauliwa, naiagiza serikali ikafanyie kazi jambo hili na ilete taarifa bungeni katika mkutano huu,” alisema.


No comments:

Post a Comment