Kagasheki: Majangili wauawe
WAZIRI
wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amewataka askari wa wanyama
pori kuhakikisha wanamalizana na majangili wa tembo pindi
wanapokutana nao porini na kwenye hifadhi za taifa.
Aidha
waziri huyo alisema kwenye kikao kijacho cha Bunge, watapeleka mabadiliko ya
sheria yatakayotoa meno zaidi kwa vyombo vya sheria kukabiliana na wimbi la
ujangili na kuongeza adhabu kwa watakaobainika au kukutwa na nyara za taifa.
Kagasheki
alitoa kauli hiyo jana jijini hapa mara baada ya
kuongoza matembezi ya kupiga vita ujangili wa tembo ambayo
yameandaliwa na Taasisi ya David Sheldrick Wildlife Trust kupitia kampeni
ya meno ya tembo.
Matembezi
hayo yaliwashirikisha wadau mbalimbali wa utalii akiwemo, Patrick Patel kutoka
Kampuni ya African Wildlife Trust aliyetembea kwa miguu kutoka Arusha hadi
Dar es Salaam akipinga ujangili wa tembo.
Kagasheki
alisema kuwa kuna majangili na kwa sasa sheria dhaifu zimechangia kwani mtu
anakamatwa akiwa na nyara za taifa halafu anaishia kupigwa faini ya fedha
kidogo.
Alisema
kuwa wanapeleka mabadiliko bungeni ili kuwezesha wale wanaopatikana na
hatia wapatiwe adhabu kubwa itakayowafanya wengine kuogopa kufanya ujangili
na kuacha biashara hiyo.
“Wana
usalama wakikutana na majangili huko kwenye porini wawamalize huko huko, tena
katika jambo hili nawaomba wale watetezi wa haki za binadamu wafunge midomo.
“Hata
hao majangili wakiwakuta watawamaliza pamoja na tembo,” alisema Kagasheki
huku umati wa watu uliokusanyika ukipiga makofi kushangilia.
Allisema
kuwa kazi ya serikali ni kuwatetea wale wasio na uwezo wa kujitetea wenyewe
kama wanyama wa porini akiwemo tembo na kwa kuwa kumekuwa na tatizo la kesi
kuchukua muda mrefu, suluhisho ni vyombo vya ulinzi kumalizana na
majangili huko huko pindi wakiwakamata.
Waziri
huyo aliongeza kuwa Tanzania imechafuka kimataifa kutokana na matukio ya
mauaji ya tembo licha ya kuongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo ikifuatiwa
na Botswana.
Pia
alikemea tabia iliyoibuka ya baadhi ya wanasiasa kutafuta ubunge na urais kwa
kutumia hifadhi jambo aliloonya kuwa likiachwa hivyo hivyo litasababisha
kuharibu uhifadhi wa wanyamapori hapa nchini.
Naye
Patrick Patel alisema kuwa matembezi ya awali aliyoyafanya kutoka Arusha hadi
Dar es Salaam yameleta hamasa kubwa kwa wananchi na ndio maana
nchi 15 duniani zimeshiriki katika matembezi ya kitaifa dhidi ya ujangili wa
tembo.
Alitaja
miji mingine iliyoshiriki matembezi hayo kuwa ni Bangkok (Thailand), Buenos
Aires (Argentina), Cape Town (Afrika Kusini), Edinburg (Scotland), London
(Uingereza), Melbourne (Australia) na Munich (Ujerumani).
Zingine
ni Nairobi (Kenya), Roma (Italia), Toronto (Canada), New York City,
Washington DC na Wellington (Marekani).
Matembezi
hayo yalianzia eneo la Majengo hadi viwanja vya AICC Kijenge na kushirikisha
wanafunzi wa shule za msingi na sekondari pamoja na wadau wa utalii.
Mwenyekiti
wa Chama cha Mawakala wa Utalii Nchini (Tato), William Chambulo, aliiomba
serikali kubadili sheria ya wanyamapori ya uwindaji wa kitalii ili
kuzuia uwindaji wa tembo.
|
No comments:
Post a Comment