Thursday, August 15, 2013

WAZIRI KAGASHEKI,MAJINA YA MAJANGILI WANAYO


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amesema kuwa wanayo majina ya wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na ujangili nchini.
Akizungumza na waandishi jana jijini Dar es Salaam katika ofisi ndogo za Bunge, Balozi Kagasheki alisema kuwa wanaojihusisha na biashara hiyo wanafahamika, na kwamba tayari jitihada mbalimbali zimeanza kuchukuliwa.
Alisema kuwa mtandao huo wa majangili kwa sasa unajulikana na kuwa wanatarajia kufanya operesheni kubwa ambayo haijawahi kutokea ili kuwanasa.
Kagasheki alisema kuwa mtandao huo unahusisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, na kuwa wapo katika mchakato wa kufuatilia nchi zinazonunua bidhaa zinazotokana na ujangili huo.
“Mtandao wa majangili kwa sasa unajulikana, tuna majina ya na tayari jitihada mbalimbali zimeanza kuchukua, hata kukamatwa kwa mfanyabiashara wa kizungu hivi karibuni ni jitihada hizo,” alisema.
Naye Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) alisema kuwa kutokana na tatizo la ujangili kuzidi kushamiri, amelazimika kuwasilisha barua ofisi ya Bunge kwa ajili ya kupeleka hoja binafsi ya kuweza kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Alisema kuwa suala hilo si dogo kama inavyofikiriwa kwa kuwa tembo wanaendelea kumalizika kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa.
“Japokuwa hoja yangu inaweza kushindwa kujadiliwa kwa kuwa suala hili linahusu watu wakubwa na wengine wenye majina. Maana niliwahi kuomba jambo hilo lifanyiwe kazi, lakini jitihada zangu ziligonga mwamba,” alisema.
Hata hivyo, Msigwa alishauri kwenda mbali zaidi ili kuibaini Kampuni ya TALL ambayo mkurugenzi wake alikamatwa na nyara za serikali.
Alisema kuwa hatua ya kukamata watu wanaokutwa na pembe za ndovu haitasaidia isipokuwa kutafuta mtandao wa wanaojihusisha na biashara hiyo na kuuweka hadharani.


No comments:

Post a Comment