Mvietnam adakwa na Meno ya
ndovu uwanja wa ndege
Kwa ufupi
Baada ya
kufanyiwa upekuzi wa kina katika begi lake alikutwa na bangili 138 na vijiti
362 vilivyotengenezwa kwa meno ya tembo.
D’Salaam.
Raia wa Vietnam, anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukutwa na shehena ya
pembe za ndovu ya kilo 19 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA).
Mtu huyo
amekamatwa wakati bado suala la watu kukamatwa na dawa za kulevya likiendelea
kurindima. Julai 5 mwaka huu, wasichana wawili Agnes Gerald (Masogange na
Melisa Edward ) walipitisha kilo 180 za dawa hizo na kwenda kukamatiwa Afrika
Kusini.
Agosti 14
mwaka huu pia mtu mmoja alikamatwa akiwa na kete 86 za dawa za kulevya aina ya
heroini na misokoto 34 ya bangi.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Deusdedit Kato alisema, raia huyo
alikamatwa juzi jioni akiwa anatokea Msumbiji na ndege ya Air Mozambique na
alikuwa katika harakati za kubadilisha ndege ili apande ndege ya Dubai.
“Jana
(juzi) majira ya saa 10:45 alasiri hapa uwanja wa ndege, alikamatwa raia wa
Vietnam akitokea Msumbiji na ndege ya Shirika la Ndege la Mozambique Airlines…
alikuwa katika harakati za kubadilisha ndege ili apate ya kwenda Vietnam
kupitia Dubai, ndipo maofisa wetu wa polisi, uwanja wa ndege na maliasili wakamshtukia,”
alisema na kuongeza: “Ilikuwa ni kwa ‘physical inspection’ (uchunguzi wa
macho), aliweza kugundulika.
Baada ya
kufanyiwa upekuzi wa kina katika begi lake alikutwa na bangili 138 na vijiti
362 vilivyotengenezwa kwa pembe za ndovu. Vyote vina uzito wa kilo 19 na
thamani ya Sh18.4 milioni.”
Hata
hivyo, alisema kuwa jitihada za kumhoji mtuhumiwa bado zinaendelea kwa kuwa
hajui lugha ya Kiswahili wala Kiingereza.
“Bado
tunatafuta mkalimani ili tumhoji kwa kina halafu atafikishwa mahakamani. Sheria
inaruhusu mtu kushtakiwa popote anapokamatiwa, siyo lazima tumrudishe Msumbiji
au kwao Vietnam,” alisema Kato. Akizungumzia hali ya ulinzi uwanjani hapo, Kato
alisema kuwa imeimarishwa na kwamba ukitokea uhalifu huwa ni wa kupangwa tu.
“Siku
zote tunawakamata wahalifu kama hawa, ikitokea kama ule mzigo wa mabegi tisa ya
dawa za kulevya, haina maana kwamba ulinzi ulilegea, watu walijua kitu
kinachoendelea. Sasa ndiyo tunajiuliza, kwa nini walijua halafu wakanyamaza,”
alisema Kato..