Mussa Juma,Mwananchi
Arusha,Serikali imetangaza kusitisha mgomo wa wapagazi wa mlima Kilimanjaro na uliotarajiwa kuanza Machi 7 mwaka huu kwa kushirikisha zaidi ya wapagazi 15,000 wa Mlima Kilimanjaro na Meru.
Wapagazi walipanga kugoma kubeba mizigo ya watalii,kupanda watalii mlima Kilimanjaro na Meru, ili kushinikiza malipo ya dola 10 kwa siku kupanda Mlima huo tofauti na malipo kati ya Tsh 6000 hadi 10,000 ambazo zinalipwa na makampuni mengi.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alitangaza uamuzi huo, baada ya kukutana na vyama vya wapagazi na vyama vya makampuni ya utalii na uongozi wa Mlima Kilimanjaro na kufikia muafaka wa kusitisha mgomo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu huyo wa mkoa alitangaza kuunda kamati maalum ya watu 20 wa sekta ya utalii kutoka mkoa wa Kilimanjaro, Arusha na wizara ya Maliasili na Utalii ili kuchunguza mgogogo huo na hatimaye kumshauri.
"ni kweli tulipokea barua ya chama cha wapagazi cha (TPO), kugoma lakini tumekaa na kujadiliana kusitisha mgomo huu ili kuipa kazi kamati maalum kuchunguza mgogoro huu"alisema Gama.
Alisema Kamati hiyo inatarajiwa kumaliza uchunguzi wake ndani ya siku 30 na baadaye atatoa maamuzi juu ya mgogoro huo wa wapagazi.
Awali Katibu Mkuu wa TPO, Mugabo Sereri alisema walitoa notisi ya siku 30 ya kufanya mgomo huo, ambayo itaisha Machi 7 siku ambayo walipanga kugoma.
Hata hivyo, alisema baada ya majadiliano na Mkuu wa mkoa wamekubaliana kusitisha mgomo huo ili kupisha uchunguzi juu ya madai ya wapagazi na matatizo mengine katika sekta ya utalii.
MWISHO
No comments:
Post a Comment